Lugha Nyingine
Maonyesho ya Canton yatangazwa katika AU ili kuunganisha biashara za Afrika na wanunuzi duniani (4)
ADDIS ABABA - Maafisa kutoka China na Umoja wa Afrika (AU) wamesisitiza umuhimu wa Maonyesho ya Uagizaji na Uuzaji Nje Bidhaa ya China, ambayo pia yanajulikana kwa jina la Maonyesho ya Canton, katika kuunganisha biashara za Afrika na wanunuzi, wawekezaji, washirika wa teknolojia, na fursa mpya za kibiashara duniani.
Kauli hiyo imetolewa kwenye mkutano uliofanyika Jumanne wiki hii katika makao makuu ya AU mjini Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, ili kutangaza Maonyesho ya 140 ya Canton.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Jiang Feng, mkuu wa Ujumbe wa China katika AU, amesema Maonyesho ya Canton yanatumika kama jukwaa muhimu la kuhimiza mabadilishano ya kiuchumi na biashara kati ya China na Afrika.
"Kupitia Maonyesho ya Canton na hatua kama vile kurahisisha taratibu za forodha na kuongeza urahisi wa biashara, China inasaidia bidhaa za Afrika zenye ubora wa hali ya juu kuingia kwenye soko la China, ikiunga mkono maendeleo ya viwanda ya Afrika na kusukuma mbele utekelezaji wa Ajenda ya AU 2063," Jiang amesema.
Huku akikumbuka kwamba Maonyesho ya 139 ya Canton yalivutia kampuni zaidi ya 22,000 na wanunuzi jumla ya 314,000 wa nje ya nchi kutoka nchi na maeneo 220, Jiang amebainisha kuwa Maonyesho ya Canton ya mwaka huu yanatarajiwa kusaidia biashara zaidi za Afrika kutafuta namna ya kuingia soko la dunia.
Ron Osman Omar, mkurugenzi wa viwanda, madini, ujasiriamali, na utalii katika Kamisheni ya AU, amesema Maonyesho ya Canton hutoa jukwaa lenye thamani kubwa la kuimarisha uhusiano wa biashara, na kupanua ushirikiano kati ya kampuni za Afrika na China.
Huku akisisitiza kwamba kampuni ndogondogo, za ukubwa mdogo, na wa ukubwa wa kati zinachukua asilimia takriban 90 ya kampuni kote Afrika, Omar amesisitiza umuhimu wa kuunganisha biashara za Afrika na soko duniani ili kuzisaidia kukua na kuwa na uwezo wa ushindani katika ngazi ya kimataifa.
"Kampuni za Afrika zinahitaji miunganisho, fedha, teknolojia, uwekezaji, ujuzi, na masoko ya kimataifa imara zaidi ili kukua na kuongeza uwezo wao. Kwa hivyo, majukwaa kama vile Maonyesho ya Canton ni muhimu sana katika kuzisaidia kuunganishwa na wanunuzi, wawekezaji na washirika wa teknolojia duniani," amesema.
Liu Xiaoguang, waziri mshauri wa Ubalozi wa China nchini Ethiopia, amesema zaidi ya biashara ya bidhaa, Maonyesho ya Canton hutoa suluhisho za uzalishaji wa ndani, vifurushi vya uwekezaji, na mafunzo ya kiufundi ili kuwezesha juhudi za maendeleo ya viwanda za Afrika.
Maonyesho ya 140 ya Canton yanatarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 23 hadi 27 mwaka huu katika Jumba la Maonyesho ya Canton mjini Guangzhou, mji mkuu wa Mkoa wa Guangdong kusini mwa China.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




