Lugha Nyingine
Nchi za Kiarabu na Kiislamu zalaani hatua za Israeli mjini Yerusalemu
AMMAN - Mawaziri wa mambo ya nje na wawakilishi wa nchi za Kiarabu na Kiislamu walikusanyika mjini Amman, Jordan jana Jumatano na kulaani kwa pamoja sera na hatua za Israeli mjini Yerusalemu na maeneo yake matakatifu.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Naibu Waziri Mkuu wa Jordan ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje Ayman Safadi ameishutumu Israeli kwa kuimarisha "ukaliaji" wake wa Yerusalemu Mashariki kwa kupitia kupanua maeneo ya makazi, kuchukua ardhi, kunyang'anya mali na kuweka vizuizi kwa Wajerusalemu.
Safadi amesema hatua hizo za Israeli zinalenga utambulisho wa Yerusalemu na historia na hali ilivyo ya sasa ya kisheria ya maeneo yake matakatifu, hasa Msikiti wa Al-Aqsa, na ameonya kwamba ukiukwaji unaoendelea unaweza kuchochea hali wasiwasi ya kidini.
Kwenye taarifa iliyopitishwa katika mkutano huo, washiriki wamelaani kile walichokielezea kuwa ni sera za Israeli zinazolenga kubadilisha utambulisho wa Waarabu, Waislamu, na Wakristo wa Yerusalemu inayokaliwa kwa mabavu. Pia wamesisitiza msimamo wao kwamba Yerusalemu Mashariki ni sehemu moja ya ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, na ni mji mkuu wa Taifa la Palestina.
Washiriki hao wametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua mara moja kuzuia hatua hizo za Israeli mjini Yerusalemu na maeneo yake matakatifu, na wamekubaliana kuanzisha mfumo, ikiwa ni pamoja na jukwaa la vyombo vya habari, ili kurekodi na kufichua vitendo vya ukiukwaji.
Mkutano huo ulihudhuriwa na mawaziri wa mambo ya nje na wawakilishi wa nchi za Kiarabu, pamoja nchi za Indonesia, Pakistan, Uturuki na Malaysia.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, maelfu ya walowezi wa Israeli, wakiambatana na maofisa wa serikali na chini ya ulinzi mkali wa polisi, waliingia kwa nguvu Msikiti wa Al-Aqsa katika Jiji la Kale la Yerusalemu Mashariki, na kusababisha ulaumu wa watu wengi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




