Lugha Nyingine
Mji wa Shanghai, China washinda tuzo ya kwanza ya WIPO ya Mji wa Uvumbuzi (2)
![]() |
| Watu wakishiriki kwenye Hafla ya Utoaji wa Tuzo ya kwanza ya WIPO ya Mji wa Uvumbuzi kwenye makao makuu ya WIPO mjini Geneva, Uswisi, Oktoba 12, 2026. (Xinhua/Lian Yi) |
GENEVA – Miji ya Shanghai nchini China, Liverpool nchini Uingereza na Charleroi nchini Ubelgiji imetangazwa na Shirika la Haki Miliki ya Ubunifu Duniani (WIPO) kuwa washindi wa tuzo ya kwanza ya WIPO ya Mji wa Uvumbuzi katika hafla ya utoaji wa tuzo hiyo iliyofanyika kwenye makao makuu ya WIPO mjini Geneva, Uswisi jana Jumatatu.
Tuzo ya WIPO ya Mji wa Uvumbuzi, ilianzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2026, iko wazi kwa miji kutoka nchi zote 194 wanachama wa WIPO na inatunukiwa kwa miji yenye maono ya kuona mbali inayotoa ahadi za kusukuma mbele uvumbuzi na ubunifu katika mwaka unaofuata. Washindi hao watatu wamechaguliwa kutoka miji 15 iliyofika hatua ya mwisho ya kuteuliwa.
Kwa mujibu wa WIPO, dira ya Shanghai ni kuimarisha nafasi yake ya kuwa kituo cha kimataifa cha sayansi, teknolojia na haki miliki ya ubunifu (IP), wakati huohuo kukuza utamaduni mpana zaidi wa uvumbuzi na ubunifu. Ahadi yake inahusisha kupanua elimu na huduma za haki miliki ya ubunifu, kufungua miundombinu ya uvumbuzi na takwimu, kuunga mkono viwanda vya ubunifu wa kitamaduni, pamoja na kuimarisha muunganisho kati ya utafiti wa kisayansi, viwanda, wajasiriamali na wawekezaji.
Zhou Yaming, Naibu Katibu Mkuu wa Serikali ya Mji wa Shanghai, amesema tuzo hiyo imeonesha Shanghai imetambuliwa sana na WIPO kwa maendeleo yake ya uvumbuzi na juhudi zake katika kujenga na kustawisha mfumo ikolojia wa haki miliki ya ubunifu.
"Pia inaonesha utambuzi wa jumuiya ya kimataifa kwa juhudi za China za kufungua mlango na kufanya uvumbuzi, ushirikiano wa kunufaishana na kutafuta mafanikio kwa pamoja," amesema.
Washindi hao wamechaguliwa na jopo huru la majaji la kimataifa lililoundwa na wataalamu wanaojulikana katika sekta za utamaduni na ubunifu, mipango ya miji, maendeleo ya maeneo ya wakazi, na ukuaji unaochochewa na uvumbuzi.
Andrea Dempster Chung, mjumbe wa Jopo hilo la Majaji la Kimataifa ambaye pia ni Mwanzilishi Mwenza na Mkurugenzi Mtendaji wa Kingston Creative, amesema ombi la Shanghai liliwapa taswira sana, na si tu kwa sababu ya msingi imara wa utafiti na maendeleo ambao mji huo tayari ulikuwa nao, bali pia kutokana na uzito wa mipango yake kabambe na nguvu ya ahadi zake.
"Hili litakuwa muhimu katika kubadilisha mustakabali wa mji huu na hii ni moja ya sababu za kwanini Shanghai imechaguliwa," amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




