Tamasha la utamaduni wa Kichina lafanyika Cairo, Misri kuadhimisha miaka 70 ya uhusiano wa kidiplomasia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 13, 2026
Tamasha la utamaduni wa Kichina lafanyika Cairo, Misri kuadhimisha miaka 70 ya uhusiano wa kidiplomasia
Mtembeleaji akijaribu sanaa ya kuchora kwa kupakaa rangi kwenye tamasha la utamaduni wa Kichina katika Chuo Kikuu cha Badr jijini Cairo, Misri, Oktoba 12, 2026. (Xinhua/Xin Mengchen)

CAIRO - Tamasha la utamaduni wa Kichina limefanyika jana Jumatatu katika Chuo Kikuu cha Badr jijini Cairo, Misri kusherehekea maadhimisho ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Misri, likishirikisha maonesho ya kitamaduni, sanaa za jadi za Kichina na programu za mabadilishano kati ya wanafunzi.

Lu Chunsheng, Waziri-Mshauri katika Ubalozi wa China nchini Misri, ameeleza matumaini yake kuwa vijana watatumia fursa hiyo kupata uelewa wa kina kuhusu kampuni na utamaduni wa Kichina na kushiriki kikamilifu katika kuimarisha urafiki kati ya China na Misri.

Amesema ubalozi wa China nchini Misri uko tayari kufanya kazi na upande wa Misri kutekeleza makubaliano muhimu yaliyofikiwa na viongozi wakuu wa nchi hizo mbili, kupanua zaidi ushirikiano katika ufundishaji wa lugha ya Kichina, elimu na utafiti wa kisayansi, kuimarisha ubadilishanaji wa walimu na wanafunzi, kuongeza kuelewana, na kuzidisha kufunzana kati ya ustaarabu wa nchi hizo.

Amr Elatraby, Makamu Rais wa Chuo Kikuu cha Badr jijini Cairo, amesema urafiki wa kudumu kati ya mataifa hauhitaji tu kuaminiana kisiasa na ushirikiano wa kiuchumi, bali pia mabadilishano katika nyanja za elimu, utamaduni na miongoni mwa vijana.

Amesema chuo hicho kinaweka umuhimu mkubwa kwenye elimu ya lugha ya Kichina na ushirikiano wa kielimu na China, na ameongeza kuwa tamasha hilo linatoa fursa kwa vijana kutoka nchi zote mbili kukutana ana kwa ana, kuongeza kuelewana na kuimarisha urafiki wao.

Wei Dong, Mwakilishi Mkuu wa Ofisi ya Kampuni ya Sinopec barani Afrika ambayo iliandaa tamasha hilo kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Badr, amesema Sinopec inaendelea kuwa na dhamira katika uendeshaji shughuli kulingana na mazingira ya nchi husika na kutimiza wajibu wake wa kijamii kwa kusaidia elimu, shughuli za kitamaduni na maendeleo ya jamii nchini Misri.

"Tamaduni za Misri na China zina sifa zake za kipekee, na ubadilishanaji wa kitamaduni umeboresha maisha yangu," Salma Hamada, mwanafunzi wa lugha ya Kichina katika Chuo Kikuu cha Badr, ameliambia shirika la habari la China, Xinhua.

Amesema vijana kutoka nchi hizo mbili sasa wana fursa zaidi za kuelewana na wanazidi kuonesha nia ya kuchangia tamaduni zao kwa uwazi na urafiki.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha