Daraja jipya la mpakani mwa China na DPRK juu ya Mto Yalu lazinduliwa rasmi (3)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 16, 2026
Daraja jipya la mpakani mwa China na DPRK juu ya Mto Yalu lazinduliwa rasmi
Picha hii iliyopigwa tarehe 15 Oktoba 2026, ikionesha daraja jipya linalovuka Mto Yalu, mto wa mpakani mwa China na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea (DPRK). (Xinhua/Pan Yulong)

SHENYANG - Daraja jipya linalounganisha China na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea (DPRK) juu ya Mto Yalu limezinduliwa na kuanza kutumika rasmi kwa usafiri wa umma jana Alhamisi, huku pande zote mbili zikifanya kwa pamoja hafla ya uzinduzi kwenye njia hiyo muhimu ya kuvuka mpaka.

Daraja hilo linaloshikiliwa kwa nyaya juu ya Mto Yalu, linatumika kama kiungo cha usafiri wa kuvuka mpaka kati ya mji wa Dandong katika Mkoa wa Liaoning, kaskazini-mashariki mwa China, na mji wa Sinuiju katika Jimbo la Pyongan Kaskazini la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea (DPRK).

Daraja hilo, lenye minara miwili na mifumo miwili ya nyaya, lina upana wa barabara wa mita 28.5 na njia nne za mielekeo miwili ya kupitisha magari kwenye pande zote mbili. Aidha, nafasi iliyoachwa chini yake kwa ajili ya kupitisha vyombo vya majini imesanifiwa kuwezesha kupita kwa vyombo vya uzito wa tani hadi 3,000.

Waziri Mkuu wa China, Li Qiang, amelisifu daraja hilo akilielezea kuwa ni alama mpya ya urafiki kati ya China na DPRK. "Daraja hili bila shaka litakuwa alama mpya inayowakilisha urafiki wa jadi kati ya China na DPRK," amesema Li katika hotuba yake iliyotolewa kwa njia ya video kwenye hafla hiyo ya uzinduzi.

Katika hotuba yake hiyo, Li ametoa wito kwa China na DPRK kutumia ufunguzi wa daraja hilo jipya kama fursa ya kuboresha taratibu za vibali vya mpakani, kuongeza muunganisho, kutumia vema uwezekano wa ushirikiano katika maeneo ya mpakani, na kuboresha ustawi wa watu wa nchi zote mbili.

Li amesema kuwa China ina nia ya kufanya kazi na DPRK kuendelea kufanya juhudi za kutekeleza makubaliano muhimu yaliyofikiwa na viongozi wakuu wa vyama na nchi hizo mbili, kuimarisha mawasiliano ya kimkakati, kuongeza kuaminiana kisiasa, kupanua ushirikiano wa kivitendo, na kuimarisha uratibu wa pande nyingi, ili kuzidisha kila mara uhusiano kati ya China na DPRK na kuleta manufaa zaidi kwa watu wa nchi zote mbili.

Daraja hilo jipya litawezesha zaidi biashara na ubadilishanaji wa kati ya watu wa nchi hizo mbili, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Mao Ning, alisema Jumatano wiki hii.

“China na DPRK ni majirani marafiki waliounganishwa na milima na mito, na daraja hili jipya ni muundombinu muhimu kwa ajili ya muunganisho kati ya nchi hizo mbili,” Mao aliuambia mkutano na waandishi wa habari.

Mji huo wa Dandong una bandari kubwa zaidi ya biashara ya mpakani kati ya China na DPRK. Kabla ya daraja hilo jipya la barabara, Daraja la Mto Yalu—linalojulikana pia kwa jina la Daraja la Urafiki kati ya China na DPRK—lilikuwa likitumika kwa ajili ya usafiri wa barabara na reli. Hata hivyo, daraja hilo la zamani liliweza kuhimili tu malori yenye uzito usiozidi tani 20 kwa safari ya mwelekeo mmoja.

Mwaka 2010, China na DPRK zilikubaliana kujenga daraja hilo jipya la barabara katika eneo la mtoni kutoka lilipo daraja hilo la zamani. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha