Yin Yuzhen, Mchina anayeongoza katika kudhibiti jangwa, atajwa miongoni mwa wanawake 100 mashujaa wa FAO (4)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 16, 2026
Yin Yuzhen, Mchina anayeongoza katika kudhibiti jangwa, atajwa miongoni mwa wanawake 100 mashujaa wa FAO
Yu Jinxiu akihudhuria hafla kwa ajili ya Wanawake 100 Mashujaa katika Mifumo ya Kilimo cha Chakula na Maendeleo ya Vijijini wa FAO, mjini Rome, Italia, tarehe 15 Oktoba 2026. (Xinhua/Wang Kaiyan)

ROME - Yin Yuzhen, Mchina anayeongoza katika kudhibiti jangwa, ametajwa miongoni mwa Wanawake 100 Mashujaa katika Mifumo ya Kilimo cha Chakula na Maendeleo Vijijini wa FAO — mpango wa kimataifa wa kutambua mchango wa watu ulioanzishwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).

Wanawake hao waliopewa heshima wamesherehekewa katika hafla iliyofanyika jana Alhamisi kwenye makao makuu ya FAO jijini Rome, ambayo ni sehemu ya Jukwaa la Chakula Duniani la mwaka huu.

Yin ametumia miongo zaidi ya minne kupambana na hali ya kuenea kwa jangwa kwenye Ardhi ya Mchanga ya Maowusu katika Mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya Ndani kaskazini mwa China. Baada ya miongo kadhaa ya kupanda miti bila kukoma, yeye na familia yake wamebadilisha maeneo makubwa ambayo hapo awali yalikuwa yasiyo na tija kuwa ardhi kubwa ya kijani, wakiyashinda mazingira magumu na mchanga unaohamahama.

Simulizi yake pia imejenga urafiki wa kudumu na mwalimu mstaafu kutoka Marekani, Ronald Sakolsky, ambaye alichangisha dola 5,000 za Marekani miongo kadhaa iliyopita ili kuunga mkono kazi yake hiyo ya upandaji miti.

Yin ameliambia shirika la habari la China, Xinhua kuwa kutambuliwa huko kumeimarisha azma yake ya kuendelea na kazi yake. "Kama farasi wa Mongolia, nitaendelea kusonga mbele kwa kustahimili magumu na azma thabiti, nikifanya kazi yangu vema na kurudisha fadhila kwa mazingira ya asili," amesema.

Akiwa miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo, macho ya Sakolsky yalikuwa yamejawa machozi ya furaha huku akipiga makofi kupongeza mafanikio hayo ya Yin. "Yin anastahili kila kitu ambacho anapata. Ni shujaa," ameliambia Xinhua.

Akihutubia hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Qu Dongyu, amesifu mchango wa wanawake wakulima. Amesema wanawake ni nguvu yenye kuchochea katika mifumo ya kilimo cha chakula, wakibeba jukumu muhimu sana katika usalama wa chakula, usimamizi wa maliasili, maendeleo ya vijijini, na kujenga uhimilivu wa jamii.

Mpango huo wa kimataifa, ulioanzishwa na FAO kuadhimisha Mwaka wa Kimataifa wa Mwanamke Mkulima 2026, unatambua wanawake 100 kwa mchango wao mkubwa katika kilimo, mifumo ya chakula na maendeleo ya vijijini.

FAO imesema ilipokea mapendekezo 609 kutoka kwa nchi wanachama wake 131, na kwamba mchakato wa uteuzi ulihusisha kuhakiki kustahiki kwa washindi, tathmini na upangaji wa nafasi za washindi uliofanywa na menejimenti ya waandamizi, pamoja na raundi mbili za majadiliano.

Mbali na Yin, Yu Jinxiu na Dong Minfang pia ni miongoni mwa Wanawake Mashujaa 100 wa FAO. Yu ni mtaalamu wa tiba ya moxibustion kutoka Wilaya ya Qichun katika Mkoa wa Hubei katikati mwa China; na Dong ni Mkuu wa Ushirika wa Kitaalamu wa Mashine za Kilimo wa Fengrui katika Wilaya ya Yueyang, Mkoa wa Hunan katikati mwa China. Wametumia miaka mingi wakichangia utaalamu wao kusaidia maelfu ya watu kupata ajira na kuanzisha biashara, jambo ambalo limeongeza mapato ya wakazi wa vijijini.

Umoja wa Mataifa uliuteua mwaka 2026 kuwa Mwaka wa Kimataifa wa Mwanamke Mkulima ili kuangazia mchango wa wanawake katika mifumo ya kilimo cha chakula, na kuhimiza sera na uwekezaji unaoboresha ufikiaji wao wa fedha, maarifa, na huduma mbalimbali.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha