Lugha Nyingine
Maonesho ya picha yafanyika katika nchi nyingi za Afrika kuadhimisha Taiwan kujitoa kutoka utawala wa kikoloni wa Japan (3)
![]() |
| Watu wakitembelea maonesho ya picha kuadhimisha miaka 81 tangu Taiwan ijitoe kutoka utawala wa kikoloni wa Japan, jijini Abuja, Nigeria, tarehe 23 Oktoba 2026. (Xinhua/Liu Jiaqi) |
NAIROBI - Maonesho ya picha kuadhimisha miaka 81 tangu Taiwan kujitoa kutoka utawala wa kikoloni wa Japan yamefanyika katika nchi tano za Afrika -- Kenya, Nigeria, Afrika Kusini, Tanzania na Msumbiji -- kuanzia tarehe 23 hadi 25 Oktoba.
Maonesho hayo yanajumuisha sehemu nne zenye mada mahsusi na kuonesha picha zaidi ya 30 chini ya kaulimbiu "Kukumbuka Taiwan Kujitoa kutoka Utawala wa Kikoloni wa Japan, Kusukuma mbele Muungano wa Kitaifa." Mabalozi wa China katika nchi husika, maafisa wa serikali za nchi husika, wanadiplomasia wa kigeni, wasomi, wawakilishi wa sekta ya biashara na wadau wa vyombo vya habari walihudhuria shughuli hizo.
Wageni walihimiza tena kuwa Taiwan ni sehemu isiyoweza kutenganishwa ya China, na kusisitiza kuwa Afrika inaunga mkono juhudi za kulinda matokeo ya ushindi wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na utaratibu wa kimataifa wa baada ya vita hivyo. Walisifu sana hatua hiyo ya kufanya maonesho kama hayo ya picha nje ya China.
Kwenye hafla ya ufunguzi wa maonesho hayo jijini Nairobi Oktoba 23, Erastus Mwencha, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, alisema kuwa Taiwan kujitoa kutoka utawala wa kikoloni wa Japan mwaka 1945 kuliashiria mwisho wa Mkataba wa Shimonoseki wa mwaka 1895 na wakati muhimu wa kurejeshwa kwa ukamilifu wa ardhi ya taifa la China.
"Umuhimu wa kihistoria wa hatua hizi unakwenda zaidi ya mipaka ya China, na pia una maana kubwa kwa Afrika," alisema.
Mwencha alikumbushia kuwa wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipopitisha Azimio No. 2758 mwaka 1971, kurejesha haki halali za Jamhuri ya Watu wa China, mataifa 26 ya Afrika yalipiga kura kuunga mkono uzimio hilo.
Siku hiyohiyo katika hafla ya ufunguzi jijini Abuja, mji mkuu wa Nigeria, Charles Onunaiju, Mkurugenzi wa Kituo cha Stadi za China, alisema uzoefu wa China wa uingiliaji wa mataifa ya nje na umwamba wa kikoloni una uhusiano wa karibu na suala la muungano wa kitaifa.
Amesema nchi za Afrika zina uzoefu wao wa kihistoria, na hivyo zina uwezo wa kuelewa msimamo wa China juu ya kulinda umoja wa kitaifa na mamlaka ya nchi.
Oktoba 24, katika hafla ya ufunguzi iliyofanyika Johannesburg, Afrika Kusini, Zheng Xingli, mkuu wa Jumuiya Kuu ya Afrika kwa ajili ya Muungano wa Amani wa China, alisema kuwa historia ni kitabu bora zaidi cha kujifunzia. Alibainisha kuwa maonesho hayo yanarejelea historia ya Taiwan kujitoa kutoka utawala wa kikoloni wa Japan kupitia mkusanyiko wa picha za kihistoria zenye thamani, na yanatoa heshima kwa wale waliojitoa mhanga na kutoa mchango katika uhuru na muungano wa taifa.
Siku hiyohiyo, hafla ya ufunguzi katika jiji la Dar es Salaam, kitovu cha biashara nchini Tanzania, Joseph Kahama, katibu mkuu wa Jumuiya ya Kuhimiza Urafiki kati ya Tanzania na China, alisema maonesho hayo yanaonesha umuhimu wa kuhifadhi kumbukumbu za kihistoria kwa ajili ya vizazi vijavyo. Alisema maonesho hayo yanatoa somo kwa Tanzania juu ya uwekaji kumbukumbu za historia, na alieleza kuunga mkono msimamo wa China juu ya muungano.
Oktoba 25, katika hafla ya ufunguzi iliyofanyika Maputo, mji mkuu wa Msumbiji, rais wa zamani wa nchi hiyo, Joaquim Chissano, alisema kuwa China imetenga rasmi tarehe 25 Oktoba kuwa Siku ya Kuadhimisha Taiwan kujitoa kutoka utawala wa kikoloni wa Japan, hatua inayoyapa maadhimisho hayo umuhimu mkubwa zaidi katika ngazi rasmi. Amesema, tarehe hiyo inabeba maana inayokwenda zaidi ya maadhimisho ya tukio la kihistoria; ikiakisi umuhimu ambao China inaweka katika kuhifadhi kumbukumbu za taifa.
Maonesho hayo ya picha, yaliyoandaliwa na Ofisi ya Kanda ya Afrika ya Shirika la Habari la China, Xinhua kwa kushirikiana na mashirika kadhaa, yataendelea kwa angalau wiki moja katika nchi hizo tano.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




