Laini ndefu zaidi ya China ya reli ya mzunguko ya metro yaanza kufanya kazi kikamilifu Wuhan (7)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 30, 2026
Laini ndefu zaidi ya China ya reli ya mzunguko ya metro yaanza kufanya kazi kikamilifu Wuhan
Wajenzi wakiwa wamepanda treni ya Laini No. 12 ya Metro ya Wuhan, mjini Wuhan, Mkoa wa Hubei, katikati mwa China, Oktoba 29, 2026. (Xinhua/Xiao Yijiu)

WUHAN – Laini No. 12 ya Treni ya Metro ya Wuhan, mji mkuu wa Mkoa wa Hubei katikati mwa China, imeanza kufanya kazi kikamilifu jana Alhamisi, na kuifanya kuwa laini ndefu zaidi ya treni ya metro ya mzunguko ya China, kwa mujibu wa Jumuiya ya Metro ya China.

Laini hiyo yenye urefu wa kilomita 59.9 na kuhudumia stesheni 37 za chini ya ardhi katika maeneo saba ya mji huo wa Wuhan, inaunganisha vituo vikuu vya reli vya Wuchang na Hankou, na inatoa fursa ya kuunganishwa na laini zingine 18 zilizopo au zilizopangwa. Mzunguko kamili huchukua dakika takriban 96.

Laini hiyo ilizinduliwa kwa awamu mbili. Sehemu ya kwanza, yenye urefu wa kilomita 35.3, ilizinduliwa na kuanza kutoa huduma tarehe 1 Mei mwaka huu. Kufuatia kuanza kufanya kazi kwa sehemu hiyo ya pili, jumla ya urefu wa mtandao wa Metro ya Wuhan sasa unazidi kilomita 581—umbali wa safari ya kuendesha gari barabarani wa takribani kati ya Berlin na Munich, au kati ya Rome na Milan.

Wuhan, inayojulikana kwa jina la "mji wa mto," ina mazingira magumu ya kijiolojia na ya maji, jambo lililosababisha changamoto mbalimbali wakati wa ujenzi. Njia hiyo inapita chini ya Mto Yangtze mara mbili na Mto Hanjiang mara moja. Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na mamlaka husika, timu za ujenzi zilishinda changamoto kadhaa za kiufundi, ikiwemo shinikizo kubwa la maji na tabaka mchanganyiko za ardhi.

Zimesema kuwa, hasa, handaki moja la kuvuka chini ya mto, lina urefu wa kilomita takriban 4, huku sehemu yake ya chini kabisa ikiwa kwenye mita 71.4 chini ya usawa wa maji ya Mto Yangtze.

“Mradi huu umetoa uzoefu muhimu kwa ajili ya ujenzi wa mahandaki yenye kipenyo kikubwa sana yanayopita chini ya mito nchini China” imeelezwa.

Mji wa Wuhan, ambao ni makazi ya wakazi wa kudumu zaidi ya milioni 13.86, ni kituo muhimu cha usafiri nchini China na mji kiini cha Ukanda wa Kiuchumi wa Mto Yangtze. Kufunguliwa kwa Laini hiyo No. 12 ya Metro kunatarajiwa kurahisisha zaidi usafiri wa umma mjini wa kuvuka mito.

Wizara ya Uchukuzi ya China ilitangaza mwezi Julai mwaka huu kuwa China imetoa mpango wa kuendeleza kwa kina maendeleo yenye sifa bora ya huduma jumuishi za usafiri katika kipindi cha Mpango wa 15 wa Miaka Mitano (2026-2030). Mpango huo unalenga kimsingi kuanzisha mfumo wa kisasa wa huduma jumuishi za usafiri ifikapo mwaka 2030.

Chini ya mpango huo, China itaboresha miunganisho miongoni mwa njia mbalimbali za usafiri, kufanya mchakato wa abiria kubadilisha laini za metro kuwa rahisi zaidi, na kuboresha huduma za usafirishaji mizigo.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Renato Lu)

Picha