Afrika Kusini yazindua cheti kwa waliopokea chanjo dhidi ya UVIKO-19

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 09, 2021
Afrika Kusini yazindua cheti kwa waliopokea chanjo dhidi ya UVIKO-19
(Picha zinatoka na Tovuti ya Shirika la Habari la China Xinhua.)

Afrika Kusini Ijumaa ya wiki hii imezindua cheti cha chanjo dhidi ya UVIKO-19 ambacho kitawawezesha wale waliopewa chanjo kuruhusiwa kupata huduma mbalimbali kama vile kuruhusiwa kuingia kwenye viwanja vya michezo.

 "Tunatarajia cheti hiki kuwa mbinu ya kuwezesha watu waliopewa chanjo kupata fursa nyingi ambazo watoa huduma mbalimbali wanatoa," alisema Waziri wa Afya Joe Phaahla wakati akizindua rasmi cheti hicho.

 Kwa miezi miwili ijayo, masuala yanayohusu usalama kwenye cheti hiki yataboreshwa, kulingana na waziri.

 "Pamoja na mambo mengine, tunatarajia maeneo ya michezo na burudani kufunguliwa zaidi kwa watu waliopewa chanjo, maduka kutoa punguzo la bei na mengine kutoa zawadi, burudani kama matamasha ya muziki kuanza kufunguliwa kwa watu waliopewa chanjo na huku hatua za usalama wa kiafya zikiendelea kuchukuliwa, sekta ya usafiri na utalii zitafunguliwa zaidi" alisema.

"Jukumu letu kama Afya ni kuwezesha kufunguliwa na kurudi taratibu kwa shughuli nyingi ambazo tumekuwa tukizikosa," alisema.

Kwa mujibu wa waziri huyo, karibu asilimia 33.4 ya watu wazima nchini Afrika Kusini wamepewa chanjo.

Phaahla alisema takwimu zinaonesha kuwa kesi za UVIKO-19 zimepungua kwa kiasi kikubwa katika wiki chache zilizopita.

"Idadi ya maambukizi mapya imekuwa yakipungua katika wiki tatu zilizopita na kupunguza asilimia 33 katika siku 7 zilizopita. Idadi ya wagonjwa wanaolazwa hospitalini imepungua kwa asilimia 19.3 katika siku 7 zilizopita. Inatia moyo zaidi kwamba idadi ya vifo vilivyoripotiwa katika siku 7 zilizopita imepungua kwa asilimia 51 hata kama kifo kimoja ni sawa na vifo vingi" alisema.  

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Renato Lu)

Picha