Viongozi wa kijeshi wa nchi tano wakutana mashariki mwa DRC kuratibu mkakati dhidi ya waasi wa M23

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 04, 2024
Viongozi wa kijeshi wa nchi tano wakutana mashariki mwa DRC kuratibu mkakati dhidi ya waasi wa M23
Wanajeshi wakionekana mjini Sake, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Machi 1, 2024. (Picha na Alain Uyakani/Xinhua)

KINSHASA, - Hali ya utulivu iko shakani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambako viongozi wa kijeshi kutoka nchi tano za kikanda za DRC, Tanzania, Malawi, Afrika Kusini na Burundi wamekuwa wakikutana kwa siku kadhaa ili kupanga mkakati wa kijeshi wa kumaliza uhasama ambao unawezekana kuongezeka kuwa mgogro wa kikanda.

Juhudi za kumaliza uhasama

Kwa siku kadhaa, viongozi hao wa kijeshi wamekuwa wakikutana mjini Goma, mji mkuu wa Jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC, ili kutathmini na kuimarisha operesheni za pamoja dhidi ya mapigano makali, hususan karibu na mji wa kimkakati wa Sake.

Mji huu unachukuliwa kuwa ngome ya mwisho kwa Goma, na ni hapa ambapo Jeshi la DRC, pamoja na washirika wake ikiwa ni pamoja na vikosi vya kijeshi vya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), vimeweka silaha nzito kuzuia kusonga mbele kwa Kundi la M23. Kundi hilo la waasi, ambalo liliibuka tena mwishoni mwa 2021, limezusha migogoro na majanga ya kibinadamu na kuteka ngome kubwa katika ardhi ya DRC, ikiwa ni pamoja na maeneo kadhaa katika milima juu ya Sake.

Lengo kuu la mkutano huu ni kushughulikia changamoto za dharura zinazoletwa na waasi wa M23 na wafuasi wao, afisa aliyehudhuria mkutano huo ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua, akisisitiza azma ya pamoja ya SADC na washirika wake kusaidia jeshi la DRC kumaliza shughuli za uasi katika eneo hilo.

Amani shakani

Wakati SADC inajipanga kwa ajili ya operesheni mashinani, hali katika eneo la Sake inaendelea kuwa tete kutokana na mashambulizi ya kila siku ya waasi wa M23 kutoka milima iliyoko juu ya mji huo.

Siku ya Alhamisi, watu wanne, akiwemo mwanajeshi mmoja wa Tanzania aliyetumwa kama sehemu ya ujumbe wa SADC, walijeruhiwa vibaya mjini Sake na mabomu yaliyorushwa na waasi hao kulenga kambi ya kijeshi na vijiji vinavyozunguka.

Serikali ya Angola imeeleza uwezekano wa kufanyika mazungumzo ya moja kwa moja kati ya rais Felix Tshisekedi wa DRC na rais Paul Kagame wa Rwanda, kufuatia mkutano wa mwisho wa Februari mjini Luanda kati ya Rais Tshisekedi na mwenzake wa Angola Joao Lourenço, ambaye ni mpatanishi mteule, kuhusu hali ya amani na usalama mashariki mwa DRC.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Deng Jie)

Picha