Mabasi yanayotumia umeme yanayoundwa nchini Ethiopia yaendeleza ajenda ya usafiri wa kijani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 02, 2024
Mabasi yanayotumia umeme yanayoundwa nchini Ethiopia yaendeleza ajenda ya usafiri wa kijani
Basi linalotumia nishati ya umeme likionekana Addis Ababa, Ethiopia, Machi 26, 2024. (Xinhua/Michael Tewelde)

ADDIS ABABA - Naol Abera alikuwa miongoni mwa abiria wa kwanza kupanda basi linalotumia nishati ya umeme kutoka eneo la uwanja wa ndege wa Bole hadi Shiro Meda huko Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia. Mabasi haya ya umeme (EV) yanaunganishwa na kukamilishwa na kampuni ya Ethiopia iitwayo Belayneh Kindie Metal Engineering Complex, kwa kutumia vipuri na sehemu za magari hayo zilizoagizwa kutoka China.

"Ni mara yangu ya kwanza kupanda basi linalotumia umeme. Nimefurahi kuona magari yanayotumia umeme yakiletwa nchini Ethiopia. Basi hilo liko vizuri sana na linasafiri haraka, na kusaidia abiria kuokoa muda," Abera amesema katika mahojiano na Shirika la Habari la China, Xinhua.

Viti vyote 44 vya basi hilo vilikuwa vimekaliwa, huku abiria sita wakiwa wamesimama hadi basi hilo la rangi ya fedha inayong'aa lilipofika kwenye kituo kinachofuata. Ilionekana kuwa wengi hawakuwa wakifahamu kuhusu huduma ya mabasi yanayotumia umeme iliyozinduliwa mwishoni mwa mwezi Machi, ambayo ni sehemu ya juhudi za Ethiopia kuendeleza usafiri wa kijani.

Kampuni ya China ya Golden Dragon hutoa vifaa hivyo kwa kampuni ya Ethiopia, ambayo inaunda sehemu za mabasi madogo ya EV na mabasi ya urefu wa mita 12 ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka nchini humo, amesema Besufekad Shewaye, meneja mkuu wa kampuni hiyo ya Ethiopia.

Serikali ya Ethiopia imeruhusu uagizaji wa vipuri na sehemu za EVs bila kutozwa ushuru ili kuhimiza matumizi ya EV na kuwezesha uhamishaji wa teknolojia katika kukabiliana na ongezeko la bei ya mafuta duniani na mabadiliko ya tabianchi.

Mwaka 2023, Ethiopia ilitumia dola bilioni sita za Kimarekani kuagiza mafuta kutoka nje, na zaidi ya nusu ya mafuta hayo yakienda kwenye magari, inasema Wizara ya Usafirishaji na Uchukuzi ya Ethiopia. Zaidi ya hayo, viwango vya uchafuzi wa mazingira katikati mwa jiji kutokana na magari haya vinaripotiwa kuwa vya kutisha.

Kuanzishwa kwa EV katika usafiri wa umma nchini humo kunakuja baada ya serikali kutangaza mipango ya kupiga marufuku uagizaji wa magari yanayotumia nishati ya petroli au dizeli ili kuharakisha mabadiliko ya uhamaji kwenda nishati mpya.

Akizungumza na Xinhua, dereva wa mabasi hayo yanayotumia umeme, Mohamed Mussa, amesema magari hayo ni rafiki kwa mazingira kwani hayana mabomba ya kutolea moshi kama mabasi ya kawaida yanayotumia petroli.

"Basi linalotumia umeme halitoi kelele au hewa ya kaboni, hivyo hakuna sauti au uchafuzi wa hewa," Mussa amesema.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha