

Lugha Nyingine
Rais wa zamani wa DRC Kabila akutana na viongozi wa kidini mjini Goma
Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Joseph Kabila (mbele) akikutana na wawakilishi wa jamii za wenyeji kwenye mkutano wao mjini Goma, mashariki mwa DRC, Mei 29, 2025. (Str/Xinhua)
GOMA, DRC - Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Joseph Kabila alijitokeza hadharani jana Alhamisi kwenye makazi yake binafsi katika Jimbo la Kivu Kaskazini, mashariki mwa nchi hiyo ambapo ameanza kukutana na wawakilishi wa jamii za wenyeji, siku chache tu baada ya kuwasili katika jimbo hilo.
"Tumekutana na Rais wa zamani Joseph Kabila kwa ombi lake ili kusikia maoni yake kuhusu hali ya sasa nchini," amesema Joel Amurani, mkuu wa kanisa la Kiprotestanti mjini Goma, baada ya mkutano huo.
Kabila aliwasili Goma, mji mkuu wa Jimbo la Kivu Kaskazini, Jumapili jioni, akiwa ameambatana na wasaidizi kadhaa wa karibu. Ziara hiyo imetokea baada ya hotuba yake ya hivi karibuni ambapo alitoa wito wa kuwepo kwa "mkataba wa wananchi" na "mwamko wa kizalendo" ili kusaidia nchi hiyo kuvuka salama kipindi hiki cha mgogoro.
Alhamisi wiki iliyopita, Baraza la Seneti la DRC lilipiga kura kuondoa kinga ya kibunge kwa Kabila, ikifungua njia ya uwezekano wa kesi za kisheria dhidi yake. Rais huyo wa zamani, ambaye aliidhinishwa kuwa seneta kwa maisha yake yote baada ya kuondoka madarakani mwaka 2019, amekuwa akishutumiwa na serikali kwa uhaini, uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu, na kushukiwa kuunga mkono kundi la waasi la M23, ambalo linaendesha operesheni zake mashariki mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa msafara wake, Kabila anatarajiwa kuendelea na mazungumzo yake leo Ijumaa na machifu wa jadi na washikadau wengine wenyeji kabla ya kuhutubia wanahabari siku zijazo.
Tangu Januari, hali ya usalama mashariki mwa DRC imekuwa ikizorota kwa kasi, kutokana na mapigano mapya yanayohusisha kundi la M23, ambayo imechukua udhibiti wa maeneo kadhaa ya kimkakati, ikiwemo miji ya Goma na Bukavu.
Kabila, ambaye alitawala nchi hiyo kutoka mwaka 2001 hadi 2019, amekuwa akiishi Afrika Kusini tangu mwaka 2023. Hivi karibuni alielezea nia yake ya kurejea nyumbani "kutoa mchango wake katika kutafuta suluhisho" kwa ajili ya kumaliza mgogoro huo unaoendelea.
Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Joseph Kabila (kushoto, mbele) akisalimiana na wawakilishi wa jamii za wenyeji kwenye mkutano wao mjini Goma, mashariki mwa DRC, Mei 29, 2025. (Str/Xinhua)
Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Joseph Kabila (kushoto, mbele) akisalimiana na wawakilishi wa jamii za wenyeji kwenye mkutano wao mjini Goma, mashariki mwa DRC, Mei 29, 2025. (Str/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma