Kuonja Chakula cha Zongzi pamoja na Kuku kwa Siku ya Duanwu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 30, 2025

Habari zenu! Mimi ni Kuku, mpenda vyakula mwenye jukumu la kufichua chakula kitamu zaidi cha kijadi cha China! Itakuwa Siku ya Duanwu tarehe 30, Mei, hebu tufungue Zongzi, chakula kitamu cha kipekee kinachoonyesha uzalendo wa Wachina.

Ikiwa inasherehekewa katika siku ya tano ya mwezi wa tano kwa kalenda ya kilimo ya China, Siku ya Duanwu, ni siku ya kwanza ya China kuorodheshwa kwenye Orodha ya Urithi wa Utamaduni Usioshikika ya UNESCO.

Kwa kupitia majani kiasi ya mianzi na wali kidogo tu, kila Zongzi inafunga ladha ya jadi na desturi ya karne nyingi. Hadithi husema kwamba kula Zongzi ni kuonyesha heshima kwa Qu Yuan, mshairi mashuhuri na waziri wa Dola ya Chu katika China ya kale, wakati wa Enzi ya Madola ya Kivita (475-221 KK).

Katika sehemu mbalimbali za China, Zongzi huja katika maumbo na ladha tofauti. Katika eneo la kusini, ni ya ladha ya chumvi —ikiwa imejazwa nyama, ute wa yai uliotiwa chumvi, au hata vyakula vya baharini. Katika eneo la kaskazini, watu wanapendelea za tamu na zenye kunata, zinazojazwa tende nyekundu, kuwekwa maharage, au mbegu za lotus. Haijalishi ni ladha gani, Zongzi ni chakula cha mezani kinachostahiki kuonjwa uhondo wake.

Kutokana na ushawishi wake wa kiutamaduni wa Siku ya Duanwu, nchi nyingi zimepitisha utamaduni wa kula Zongzi. Nchini Japan, Zongzi huitwa chimaki na hutengenezwa kwa unga wa mchele wa kusagwa. Zongzi za Malaysia (Nyonya chang) zina rangi ya buluu isiyokoza, zikipikwa kwenye maziwa ya nazi, na zikiwa zimejaa ladha ya Asia Kusini-Mashariki.

Nchi nyingi pia zina chakula kinachofanana na Zongzi, ikiwemo tamales ya Mexico, dolmadakia ya Ugiriki, na pamonha ya Brazili, na kadhalika.

Zongzi si desturi pekee ya Siku ya Duanwu hata hivyo! Siku hiyo ina desturi nyingine nyingi, zikiwemo za mashindano ya mbio za mashua za dragoni, kuning'iniza koga na mibuyu kwenye milango, na kuvaa nyuzi za hariri za rangi tano. Mashindano ya mbio za mashua za Dragoni hata yamekuwa mchezo wa kimataifa, ukijipatia mashabiki kote duniani.

Hivyo katika siku hii maalum, hebu tule Zongzi pamoja na kufurahia pamoja! Ninawatakia nyinyi nyote amani, afya njema na Siku yenye furaha ya Duanwu!

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha