

Lugha Nyingine
China yasema Marekani imeharibu vibaya makubaliano yaliyofikiwa wakati wa mazungumzo ya Geneva
BEIJING - Wizara ya Biashara ya China imesema jana Jumatatu kwamba Marekani imeharibu vibaya makubaliano yaliyofikiwa wakati wa Mazungumzo ya uchumi na biashara kati ya China na Marekani mjini Geneva, ikichukua hatua mbalimbali za vizuizi vya kubagua dhidi ya China.
Msemaji wa wizara hiyo amesema, hatua hizo zikiwa pamoja na kutoa mwongozo wa udhibiti wa uuzaji nje chipu za AI, kusitisha uuzaji wa programu ya kutengeneza chipu kwa China, na kutangaza kufutwa kwa viza kwa wanafunzi wa China.
“Vitendo hivi vimekiuka sana maoni ya pamoja yaliyofikiwa wakati wa mazungumzo ya simu kati ya wakuu wawili wa nchi hizo mbili Januari 17 na vimedhuru vibaya haki na maslahi halali ya China,” amesema msemaji huyo.
Msemaji huyo amesema, Marekani imezusha mara kwa mara mkwaruzano mpya wa kiuchumi na kibiashara kwa upande wake mmoja, ikizidisha hali ya kutokuwa na uhakika na utulivu katika uhusiano wa kiuchumi na kibiashara wa pande mbili.
"Badala ya kutafakari juu ya hatua zake yenyewe, Marekani bila msingi wowote imeishutumu China kwa kukiuka makubaliano, madai ambayo yanapotosha ukweli wa mambo. China inakataa kithabiti shutuma hizi zisizo na msingi," msemaji huyo amesema.
Msemaji huyo amesema kuwa China imefuta au kusitisha kwa muda hatua husika za ushuru na zisizo za kiushuru zilizopitishwa dhidi ya "ushuru wa kulipizana," China imechukua hatua kwa kuwajibika, ikichukulia makubaliano yaliyofikiwa katika mazungumzo ya Geneva kwa uzito, ikiyatekeleza kwa umakini, na kuyashikilia kwa juhudi.
"China inalinda haki na maslahi yake kwa msimamo imara, na kutekeleza makubaliano kwa udhati," amesema msemaji huyo.
Msemaji huyo amesema, matokeo ya mazungumzo ya Geneva "yalipatikana kwa juhudi ngumu," ameihimiza Marekani kufanya juhudi za pamoja na China kwa mwelekeo mmoja, na kurekebisha mara moja vitendo vyake potofu, ili kushikilia kwa pamoja makubaliano ya mazungumzo, na kuhimiza maendeleo mazuri, tulivu na endelevu ya uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Marekani.
“Kama upande wa Marekani utashikilia kufuata njia hiyo potofu na kuendelea kudhuru maslahi ya China, China itachukua kithabiti hatua kali kulinda haki na maslahi yake halali,” amesisitiza msemaji huyo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma