Umoja wa Mataifa walaani shambulio dhidi ya msafara wa msaada nchini Sudan

(CRI Online) Juni 04, 2025

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amelaani vikali shambulio lililosababisha vifo vya wafanyakazi watano waliokuwa katika msafara wa magari ya msaada ya Umoja huo nchini Sudan.

Dujarric amesema watu wengine kadhaa wamejeruhiwa katika shambulio hilo lililotokea Jumatatu usiku dhidi ya msafara wa magari zaidi ya 30, yakiwemo malori 15 ya Shirika la Mpango wa Chakula na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa ambayo yalikuwa yamebeba chakula na bidhaa za lishe.

Amesema taarifa juu ya msafara huo zilitolewa mapema na pande zote husika zilifahamishwa na zilifahamu sehemu malori hayo yalipokuwa, na kuongeza kuwa, malori kadhaa yamechomwa moto na vifaa vya misaada ya kibinadamu kuharibiwa.

Ametoa wito kwa mazingira salama, na ya uhakika ya kutekeleza operesheni, na kuheshimiwa kwa sheria ya kibidanadamu ya kimataifa na pande zote, si nchini Sudan pekee, bali katika nchi zote zinaoathiriwa na mapigano.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha