

Lugha Nyingine
Marekani yaipigia kura ya veto mswada wa azimio la Baraza la Usalama la usimamishaji vita mara moja huko Gaza
Kaimu Mwakilishi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Dorothy Shea (katikati, mbele) akipiga kura ya hapana kwa mswada wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Juni 4, 2025. (Xinhua/Xie E)
UMOJA WA MATAIFA – Marekani imeipigia kura ya hapana kwa mswada wa azimio la Baraza la Usalama kuhusu usimamishaji mara moja wa vita mjini Gaza na kuondolewa mara moja kwa vizuizi vyote vya misaada ya kibinadamu ambapo mswada huo wa azimio, lililowasilishwa na wajumbe 10 waliochaguliwa wa Baraza hilo, limepata uungwaji mkono wa nchi wajumbe 14 kati ya 15 huku Marekani, ambayo inashikilia haki ya kura ya veto, ikipiga kura kulipinga.
Mswada wa azimio hilo ambalo linataka kuachiliwa mara moja na bila masharti mateka wote wanaoshikiliwa na Hamas na makundi mengine, na kuondolewa mara moja na bila masharti vizuizi vyote vya kuingia kwa misaada ya kibinadamu Gaza na usambazaji wake salama na usiozuiliwa kwa kiwango kikubwa.
Kura hiyo ya hapana ya Marekani imekosolewa na nchi wanachama wa Baraza la Usalama.
Fu Cong, mjumbe wa kudumu wa China kwenye Umoja wa Mataifa, amesema China imesikitishwa sana na matokeo ya kura hiyo ya Jumatano, akisema kuwa mswada wa azimio hilo inahusu mahitaji ya haraka zaidi ya watu mjini Gaza na inaonyesha sauti ya walio wengi ya jumuiya ya kimataifa.
"Marekani kwa mara nyingine tena imetumia vibaya haki zake za kura ya veto, ikizima mwanga wa matumaini kwa watu mjini Gaza na kuendelea kuwaacha watu zaidi ya milioni 2 gizani. Ni lazima ikabiliane na maswali kutoka jumuiya ya kimataifa," amesema.
Balozi wa Uingereza katika Umoja huo, Barbara Woodward amesema nchi yake imepiga kura kuunga mkono mswada wa azimio hilo kwa sababu hali isiyovumilika mjini Gaza inahitaji kumaliza.
"Maamuzi ya serikali ya Israel ya kupanua operesheni yake ya kijeshi mjini Gaza na kuzuia kwa kiasi kikubwa misaada katika ukanda huo hayakubaliki, hayana uwiano, na matokeo yake ni mabaya na serikali ya Uingereza inayapinga kabisa," amesema.
Amesema, Uingereza inaunga mkono wito wa Umoja wa Mataifa wa kufanya uchunguzi huru mara moja kuhusu matukio haya na wahusika kuwajibishwa, akiongeza kuwa Israel inahitaji kukomesha vizuizi vyake vya misaada na kuruhusu chombo hicho cha dunia kutekeleza shughuli zake za kibinadamu mjini Gaza.
Balozi wa Algeria kwenye Umoja wa Mataifa, Amar Bendjama amesema mswada wa azimio hilo haikuwa sauti ya wachache, bali ni nia ya pamoja ya dunia nzima.
"Ni ujumbe kwa watu wa Palestina: hamko peke yenu. Na ni ujumbe kwa mkaliaji kimabavu Israel: dunia imekutazama. Ngao ya kupuuza, ya kinga lazima ianguke," amesema.
Wajumbe wakipiga kura juu ya mswada wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Juni 4, 2025. (Xinhua/Xie E)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma