"Olimpiki ya Mvinyo" yarejea China wakati wa kufunguliwa kwa maonyesho ya mvinyo ya kimataifa (2)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 10, 2025
Picha hii iliyopigwa kwa droni Juni 9, 2025 ikionyesha mwonekano wa mabanda yote ya Maonyesho ya Mivinyo Duniani wakati wa kufunguliwa kwa Maonyesho ya Tano ya Kimataifa ya Utamaduni wa Mvinyo na Utalii ya Ningxia, China huko Yinchuan, Mkoa unaojiendesha wa Ningxia, Kaskazini-magharibi mwa China. (Xinhua/Wang Peng)

YINCHUAN - Maonyesho ya Tano ya Kimataifa ya Utamaduni wa Mvinyo na Utalii ya Ningxia, China yamefunguliwa jana Jumatatu huko Yinchuan, mji mkuu wa Mkoa unaojiendesha wa Kabila la Wahui wa Ningxia, kaskazini magharibi mwa China, huku Maonesho ya Concours Mondial de Bruxelles (CMB) – ambayo pia huitwa "Olimpiki ya Mvinyo" -- yakirejea China baada ya miaka saba.

Maonyesho hayo ya siku nne yamevutia wageni zaidi ya 1,100 wa ndani na nje ya China, yakihusisha shughuli 14 kama vile maonyesho ya mashamba ya mvinyo na maonesho ya mvinyo, mashindano ya uvumbuzi, na maonyesho makubwa ya sanaa ambayo yanafanyika kila baada ya miaka miwili.

Mwenyekiti wa CMB Baudouin Havaux amesema, 'olimpiki ya mvinyo' ilifanyika kwa mara yake ya kwanza Beijing, China mwaka 2018, mwaka huu imekutanisha pamoja majaji karibu 400 wa kimataifa na sampuli zaidi ya 7,000 za mvinyo, zikiwemo za idadi ya mvinyo wa China inayovunja rekodi kwenye mashindano.

"Maonesho hayo yanafungua zama mpya kwa mvinyo wa China kujulikana duniani," Havaux amesema.

Ameongeza kuwa si kwa bahati kwamba CMB ya 32 inafanyika Yinchuan, kwani inaonyesha kidhahiri nguvu inayoongezeka ya mvinyo wa China, hasa ule kutoka Ningxia.

Mkoa huo unajivunia mazingira ya asili ya kipekee kwa kutengeneza mvinyo wa hali ya juu, mazingira hayo yenye mwanga wa jua wa muda mrefu na tabianchi ya baridi na kavu yanasaidia kilimo cha zabibu. Baada ya miongo minne ya maendeleo, Ningxia umekuwa eneo kubwa zaidi kwa kuzalisha mvinyo wa China. Sehemu ya mashariki ya Mlima Helan inasifiwa na watu wengi kuwa "eneo la dhahabu" kwa ukuzaji wa zabibu na uzalishaji wa mvinyo wa hali ya juu.

Hadi kufikia mwisho wa mwaka wa 2024, Ningxia ilikuwa na mashamba ya zabibu ya hekta 40,000 hivi ya kutengeneza mvinyo, na uzalishaji wa mwaka wa mvinyo wa chupa milioni 140. Mvinyo wake unasafirishwa kuuzwa nje kwa nchi na maeneo zaidi ya 40.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha