

Lugha Nyingine
Mafuriko yalazimisha wanafunzi zaidi ya 400 kuhamishwa kabla ya mtihani muhimu kusini mwa China (2)
NANNING - Wanafunzi zaidi ya 400 wa darasa la tisa na walimu 30 wamehamishwa jana Jumatatu, siku moja kabla ya mtihani wa kujiunga na shule ya sekondari ya juu, wakati siku za mvua kali zikisababisha mafuriko kwenye eneo la kufanyia mtihani huo katika Mkoa unaojiendesha wa Kabila la Wazhuang wa Guangxi, kusini mwa China.
Shule ya Sekondari ya Juu ya Kikabila ya Wilaya ya Tian'e, iliyoko katika eneo la uwanda wa chini la Wilaya ya Tian'e, imeshuhudia mafuriko makubwa kuanzia Jumapili, yakilazimu uhamishaji wa awali hadi kwenye mabweni ya ghorofa ya pili na jengo la darasa majira ya saa 10 alfajiri jana Jumatatu.
Wanafunzi na walimu hatimaye walihamishiwa hadi shule nyingine katika wilaya hiyo kama mahali mbadala pa kufanyia mtihani baadaye siku hiyo ya Jumatatu asubuhi huku mvua ikinyesha.
Kwa mujibu wa utabiri wa hali ya hewa, mvua zaidi zitanyesha katika siku tatu zijazo.
Mtihani huo wa kujiunga na shule ya sekondari ya juu umepangwa kufanyika kuanzia leo Jumanne hadi Alhamisi, wakati wanafunzi zaidi ya 2,200 katika wilaya hiyo wakiwa wamejiandikisha kufanya mtihani huo.
Msimu wa mvua unapowadia, Mamlaka ya Hali ya Hewa ya China imetoa tahadhari ya rangi ya chungwa kwa dhoruba za mvua na tahadhari nyekundu kwa mafuriko ya milimani Ijumaa wiki iliyopita, ikitabiri mvua kunyesha mfululizo katika baadhi ya sehemu za China, ukiwemo mkoa huo wa Guangxi, kufikia Jumatatu.
China ina mfumo wa tahadhari za hali ya hewa wa madaraja manne, ulio na ishara za rangi, huku nyekundu ikiwakilisha tahadhari kali zaidi, ikifuatiwa na rangi ya chungwa, njano na buluu.
Kuendeleza urithi wa utamaduni usioshikika wa China - ustadi wa kutengeneza chai ya Taiping Houkui
Njia mpya za uendeshaji wa droni zaanza kutumika katika Mji wa Wuhan katikati mwa China
Shughuli za utalii za siku za lavender zahimiza maendeleo ya uchumi katika Mkoa wa Xinjiang, China
Wajenzi waendelea kujenga daraja refu zaidi duniani katika Mkoa wa Guizhou wa China
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma