Mafuriko yalazimisha wanafunzi zaidi ya 400 kuhamishwa kabla ya mtihani muhimu kusini mwa China (4)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 24, 2025
Mafuriko yalazimisha wanafunzi zaidi ya 400 kuhamishwa kabla ya mtihani muhimu kusini mwa China
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Juu ya Kikabila ya Wilaya ya Tian'e wakiwa wamepumzika kwenye bweni la shule nyingine katika Wilaya ya Tian'e ya Hechi, Mkoa unaojiendesha wa Kabila la Wazhuang wa Guangxi, kusini magharibi mwa China, Juni 23, 2025. (Picha na Ao Xuelian/Xinhua)

NANNING - Wanafunzi zaidi ya 400 wa darasa la tisa na walimu 30 wamehamishwa jana Jumatatu, siku moja kabla ya mtihani wa kujiunga na shule ya sekondari ya juu, wakati siku za mvua kali zikisababisha mafuriko kwenye eneo la kufanyia mtihani huo katika Mkoa unaojiendesha wa Kabila la Wazhuang wa Guangxi, kusini mwa China.

Shule ya Sekondari ya Juu ya Kikabila ya Wilaya ya Tian'e, iliyoko katika eneo la uwanda wa chini la Wilaya ya Tian'e, imeshuhudia mafuriko makubwa kuanzia Jumapili, yakilazimu uhamishaji wa awali hadi kwenye mabweni ya ghorofa ya pili na jengo la darasa majira ya saa 10 alfajiri jana Jumatatu.

Wanafunzi na walimu hatimaye walihamishiwa hadi shule nyingine katika wilaya hiyo kama mahali mbadala pa kufanyia mtihani baadaye siku hiyo ya Jumatatu asubuhi huku mvua ikinyesha.

Kwa mujibu wa utabiri wa hali ya hewa, mvua zaidi zitanyesha katika siku tatu zijazo.

Mtihani huo wa kujiunga na shule ya sekondari ya juu umepangwa kufanyika kuanzia leo Jumanne hadi Alhamisi, wakati wanafunzi zaidi ya 2,200 katika wilaya hiyo wakiwa wamejiandikisha kufanya mtihani huo.

Msimu wa mvua unapowadia, Mamlaka ya Hali ya Hewa ya China imetoa tahadhari ya rangi ya chungwa kwa dhoruba za mvua na tahadhari nyekundu kwa mafuriko ya milimani Ijumaa wiki iliyopita, ikitabiri mvua kunyesha mfululizo katika baadhi ya sehemu za China, ukiwemo mkoa huo wa Guangxi, kufikia Jumatatu.

China ina mfumo wa tahadhari za hali ya hewa wa madaraja manne, ulio na ishara za rangi, huku nyekundu ikiwakilisha tahadhari kali zaidi, ikifuatiwa na rangi ya chungwa, njano na buluu.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha