

Lugha Nyingine
China yarusha chombo cha kubebea mizigo cha Tianzhou-9 kupeleka mahitaji kwenye kituo cha anga ya juu
WENCHANG, Hainan - Shirika la Vyombo vya Anga ya Juu la China limesema, China imerusha chombo cha kubeba mizigo cha Tianzhou-9 leo Jumanne asubuhi mapema kwa kupeleka vitu vya mahitaji kwa ajili ya kituo chake cha anga ya juu cha Tiangong kilicho kwenye obiti, ambapo roketi ya Long March-7 Y10, iliyobeba chombo hicho cha Tianzhou-9, imerushwa saa 11:34 alfajiri (saa za Beijing) kutoka Eneo la Kurushia Vyombo Kwenda Anga ya Juu la Wenchang, Mkoa wa Hainan, Kusini mwa China.
Shirika hilo limesema, dakika 10 hivi baada ya hapo, chombo hicho cha Tianzhou-9 kilijitenga na roketi hiyo na kuingia kwenye obiti yake iliyopangwa mapema na paneli zake za jua zilifunguliwa punde.
Shirika hilo limetangaza urushaji huo umepata mafanikio kamili.
Shirika hilo limesema, chombo hicho cha mizigo baadaye kitafanya minyumbuliko na kutia nanga kuunganishwa na kituo cha anga ya juu.
Chombo hicho cha Tianzhou-9 kimepakiwa mahitaji muhimu, yakiwemo vitu vya matumizi kwa wanaanga walio kwenye obiti, propela, na vifaa kwa ajili ya matumizi ya majaribio na vipimo vya kisayansi.
Jukumu hilo ni safari ya nne ya usambazaji mizigo ya mradi wa kurusha vyombo kwenda anga ya juu wa China tangu kituo hicho kiingie katika awamu ya matumizi na uendelezaji. Pia ni safari ya 584 ya mfululizo wa roketi ya Long March.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma