

Lugha Nyingine
UM walaani kuongezeka kwa mashambulio dhidi ya raia mashariki mwa DRC
Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volkner Turk amelaani kuongezeka kwa mashambulio dhidi ya raia yanayofanywa na kundi la waasi la M23 na makundi mengine yenye silaha mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika mwezi mmoja uliopita.
Kwa mujibu wa ripoti zilizopokelewa na Ofisi ya Kamishna wa Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR), kati ya tarehe 9 na 21 Julai, raia 319 waliuawa na kundi la M23 katika vijiji vinne vilivyoko Rutshuru, mkoa wa Kivu Kaskazini, wengi wao wakiwa wakulima walioweka kambi katika mashamba yao wakati wa msimu huu wa kilimo.
Pia Ofisi hiyo imepokea ripoti ya mashambulio kadhaa dhidi ya raia yaliyofanywa na makundi yenye silaha katika mikoa ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri mwezi uliopita.
Katika taarifa yake, Turk ametoa tena wito kwa pande zote zinazohusika na mgogoro huo mashariki mwa DRC kulinda raia, na kudumisha wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu na sheria ya kimataifa ya haki za binadamu.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma