

Lugha Nyingine
Kenya kutumia ipasavyo maeneo maalum ya kiuchumi kusaidia msingi wa viwanda na kuongeza mauzo ya nje
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda ya Kenya Abubakar Hassan Abubakar amesema nchi hiyo inapanga kutumia maeneo maalum ya kiuchumi ili kuimarisha msingi wa viwanda na kuongeza mauzo ya nje.
Abubakar alisema hayo Jumatano wakati wa uzinduzi wa Maeneo Maalum ya Kiuchumi ya Kifaru Exim yaliyoko katika Tatu City, takriban kilomita 20 kaskazini mwa Nairobi, akiongeza kuwa Kenya imetenga maeneo maalum ya kiuchumi yanayomilikiwa na umma na watu binafsi ambayo yanatoa motisha za kifedha na kiutawala kwa wawekezaji wa ndani na nje. Maeneo hayo yana fursa ya kutoa jukwaa la ongezeko la thamani la kupanua uzalishaji katika sekta ya kilimo, dawa na nguo. Amebainisha kuwa maeneo hayo kama vitovu shindani vya utengenezaji, yataiwezesha Kenya kupata mikataba mingi ya upendeleo ya kibiashara inayosainiwa na washirika wa kibiashara ili kukuza mauzo ya nje.
Mkuu wa idara ya huduma za maendeleo ya biashara katika Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Kiuchumi Victor Mageto amesema kuwa Kenya inatekeleza mageuzi ili kurekebisha kanuni na kupunguza vikwazo vya ukiritimba pamoja na gharama ya kufanya biashara.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma