Mji wa Tianjin wa China wazindua njia ya treni za mizigo ya kuvuka Bahari ya Caspian hadi Azerbaijan

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 20, 2026
Mji wa Tianjin wa China wazindua njia ya treni za mizigo ya kuvuka Bahari ya Caspian hadi Azerbaijan
Picha hii iliyopigwa Januari 19, 2026 ikionyesha treni ya kwanza ya mizigo ya kuvuka Bahari ya Caspian inayosafirisha bidhaa kati ya China na Asia ya Kati ikifunga safari kutoka Mji wa Tianjin, kaskazini mwa China. (Xinhua/Li Ran)

TIANJIN - Treni ya kwanza ya mizigo ya kuvuka Bahari ya Caspian inayosafirisha bidhaa kati ya China na Asia ya Kati kutoka Mji wa Tianjin kaskazini mwa China hadi Baku, Azerbaijan, imefunga safari jana Jumatatu, ikibeba bidhaa kama vile mabomba ya chuma cha pua na vifaa vya nyumbani vya kutumia umeme.

Treni hiyo chini ya uendeshaji wa Kundi la Reli la China tawi la Beijing (China Railway Beijing Group), itavuka mpaka wa China kupitia Bandari ya Horgos katika Mkoa Unaojiendesha wa Kabila la Wauygur wa Xinjiang kaskazini magharibi mwa China kabla ya kupitia Kazakhstan na hatimaye kusafirishwa kwenye meli kuvuka Bahari ya Caspian hadi Baku.

"Njia hiyo mpya inaongeza njia ya usafiri wa treni za mizigo iliyo tulivu na yenye ufanisi wa juu kati ya Tianjin na Azerbaijan, Kazakhstan na nchi nyingine," amesema Yang Junyong kutoka Kituo cha Makontena cha Tianjin.

Yang amesema, umbali wa usafiri wa njia hiyo ni wa kilomita takriban 7,000 na kwa siku 20 hivi, inapunguza muda wa usafiri kwa siku 10 hivi ikilinganishwa na usafiri wa kawaida kwenye njia ya baharini.

Baku, mji mkuu wa Azerbaijan, ni kituo muhimu kwenye ushoroba wa kimataifa wa usafirishaji wa njia mbalimbali wa kuvuka Caspian. Baada ya treni hiyo kuwasili kutoka Tianjin, bidhaa zinaweza kusambazwa tena hadi sehemu nyingine kutoka Baku.

Mwaka 2025, stesheni hiyo iliendesha jumla ya treni 390 za mizigo za China-Ulaya (Asia ya Kati), na kufikia ongezeko la asilimia 38 ikilinganishwa na mwaka 2024.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha