Wapalestina 11 wauawa kwa mashumbuizi ya Israeli katika Ukanda wa Gaza, Israeli imesema ililenga washukiwa wa Hamas (3)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 23, 2026
Wapalestina 11 wauawa kwa mashumbuizi ya Israeli katika Ukanda wa Gaza, Israeli imesema ililenga washukiwa wa Hamas
Waombolezaji wakihudhuria mazishi ya waandishi wa habari watatu wa Palestina, ambao wameuawa kwa shambulizi la anga la Israeli juzi Jumatano, katika mji wa Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza, Januari 22, 2026. (Picha/VCG)

GAZA/JERUSALEM – Vyanzo vya Palestina vimesema kuwa Wapalestina kumi na mmoja wameuawa kwa mashambulizi ya Israeli Jumatano wiki hii katika maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Gaza huku mvutano ukizidi kuongezeka.

Shambulizi la droni la Israeli lililenga gari la raia karibu na Hospitali ya Uturuki katika mji wa al-Zahra katikati mwa Gaza, vyanzo vya habari na mashuhuda wa eneo hilo wamesema, huku wakieleza kuwa gari hilo lilikuwa limewabeba wapiga picha Wapalestina waliokuwa wakifanya kazi na Kamati ya Misri ya Misaada kwa Ukanda wa Gaza.

Mahmoud Bassal, msemaji wa Idara ya Ulinzi wa Raia ya Gaza, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba shambulizi hilo liliua watu watatu -- Mohammed Qashta, Abdul Raouf Shaath, na Anas Ghneim -- wote wakiwa wafanyakazi wa vyombo vya habari, na kuwajeruhi wengine kadhaa.

Baadaye siku hiyo, Jeshi la Israeli lilisema katika taarifa kwamba shambulizi hilo lililenga "washukiwa kadhaa waliokuwa wakiendesha droni inayohusishwa na Hamas."

"Shambulizi hilo lilifanywa kwa mujibu wa utaratibu wa idhini ya amri inayohitajika," taarifa hiyo imesema, ikiongeza kuwa tukio hilo bado linapitiwa.

Bassal amesema, katika tukio lingine watu watatu waliuawa na makombora ya Israeli yaliyorushwa katika maeneo ya mashariki mwa kambi ya wakimbizi ya al-Maghazi katikati mwa Gaza, ambapo miili yao imehamishiwa hospitali iliyo karibu.

“Watu wengine watatu, akiwemo mtoto mmoja, waliuawa kwa kufyatuliwa risasi na makombora mashariki mwa Deir al-Balah katikati mwa Gaza,” amesema, akiongeza kuwa mvulana wa miaka 13 na mwanamke wa miaka 32 waliuawa katika shambulizi la Israeli huko Khan Younis, kusini mwa Gaza.

Wakati huo huo, vyanzo vya usalama vya Palestina vimeliambia Xinhua kwamba ndege za Israeli zilifanya mashambulizi matatu ya anga katika mji wa Bani Suheila, mashariki mwa Khan Younis, na mengine matatu katikati mwa Gaza, huku helikopta na makombora pia yakilenga maeneo ya karibu na Khan Younis na magharibi mwa Rafah.

Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) limesema katika taarifa ya Jumatano kwamba "Wanajeshi wa IDF katika Kamandi ya Kusini wanaendelea kuwekwa kwa mujibu wa makubaliano ya kusimamisha mapigano na wataendelea kuchukua hatua ili kuondoa tishio lolote la haraka."

Hamas Jumatano iliishutumu Israeli kwa kutumia vibaya kimakusudi kushindwa kupatikana kwa mwili wa mateka wa mwisho wa Israeli katika Ukanda wa Gaza kama kisingizio cha kukwepa majukumu yake chini ya kipindi cha kwanza cha makubaliano ya kusimamisha mapigano.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha