Lugha Nyingine
Raia wa DRC bado waendelea kuteseka mwaka mmoja baada ya Mji wa Goma kutekwa na M23 (5)
![]() |
| Askari wa kundi la M23 akifanya doria mjini Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Januari 27, 2026. (Str/Xinhua) |
GOMA, DRC - Mwaka mmoja baada ya Mji wa Goma, kitovu cha miji ya kikanda mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kutekwa na kundi la waasi la Vuguvugu la Machi 23 (M23), mgogoro huo unaendelea kuathiri maisha ya kila siku katika eneo hilo.
Katika saa za mapema Januari 27, 2025, waasi hao wa M23 walichukua udhibiti wa sehemu kubwa za mji wa Goma, ambao pia ni mji mkuu wa Jimbo la Kivu Kaskazini, na una wakazi takriban milioni mbili, baada ya mapigano makali na vikosi vya serikali.
Kwa wengi, mshtuko wa siku hiyo bado uko wazi akilini mwa wengi. Parfait Famba, mkazi, anakumbuka akiamshwa na sauti za silaha nzito kote mjini humo.
"Kati ya saa 5:00 asubuhi na mchana, hali ilizidi kuwa mbaya sana kwa kasi, na kila mmoja alilazimika kubaki amejifungia ndani ya nyumba zao," amesema.
"Tulikuta miili karibu kila mahali. Hakukuwa na njia ya kupita. Tuliogopa sana kiasi kwamba tulibaki ndani kwa karibu wiki nzima. Nilidhani sote tungekufa." Famba amesema.
Zaidi ya vurugu za mara moja, mgogoro huo umeharibu maisha ya kila siku. Kufungwa kwa muda mrefu kwa uwanja wa ndege na benki kumezidisha kutengwa kiuchumi kwa mji huo, hali iliyosukuma miamala na shughuli za kila siku za kujipatia riziki kwenye ukingo wa kusambaratika.
"Biashara karibia itasimama kabisa. Bila benki na safari za ndege za mara kwa mara, kila kitu kimekuwa ghali zaidi." amesema Adeline Muhanzi, mfanyabiashara wa kuuza bidhaa dukani katika mji huo.
Kusafiri hadi mji mkuu wa DRC, Kinshasa, sasa kunahitaji kusafiri kupitia Uganda au Rwanda kwa ndege za kimataifa -- chaguo ambalo kifedha haliwezi kufikiki kwa idadi kubwa ya wakazi.
Sylvain Kasidika ameielezea hali hiyo kuwa ni utulivu dhaifu unaofunikwa na ugumu mkubwa wa kiuchumi.
"Tunateseka sana kwa sababu hakuna mzunguko wa fedha mjini. Jumuiya na mashirika karibu yote ambayo yalikuwa yakitoa pesa hayafanyi kazi tena. Uwanja wa ndege bado umefungwa, na hakuna benki," amesema Kasidika.
Kwa mujibu wa Paul Kashanvu, mkaazi mwenyeji aliyejeruhiwa na mapigano, siri ya uwezo wa Goma kustahimili hali ngumu ni ujasiri, akili, na kupunguza gharama.
"Mahali ambapo tulikuwa tukitumia faranga 1,000 (dola 0.44 za Marekani), sasa tunatumia faranga 500. Mahali tulipokuwa tukila samaki, sasa tunakula mboga," amesema.
Kwenye maeneo ya mashinani, uwepo wa waasi umeimarishwa sana karibu na Goma, haswa katika maeneo ya Rutshuru, Masisi, na Nyiragongo katika Jimbo la Kivu Kaskazini.
Katika Mji wa Goma, kundi la M23 linadhibiti kivuko kikuu cha mpaka na Rwanda, vilevile kituo cha mpakani cha Bunagana kinachounganisha Uganda, ambavyo ni vituo vya usafiri vinavyokadiriwa kuzalisha mamia ya maelfu ya dola za Marekani kwa mwezi.
Kwa mujibu wa ripoti ya Kundi la Wataalamu la Umoja wa Mataifa iliyochapishwa Desemba 2025, M23 imeendelea kupanua udhibiti wake juu ya maeneo ya kimkakati ya uchimbaji madini katika Jimbo la Kivu Kusini, ikiimarisha upatikanaji wake wa rasilimali za madini zinazofadhili shughuli zake za kijeshi.
Serikali ya DRC imelaani hali hiyo, ikiielezea kuwa ni "uvamizi haramu na jaribio la kuhalalisha kundi lenye silaha linaloungwa mkono na nguvu za nje," amesema Patrick Muyaya, msemaji wa serikali.
Kwa upande wake, M23 imetoa taarifa Jumatatu wiki hii ikisisitiza kwamba "haitajiondoa kutoka kwenye eneo lolote katika maeneo yaliyokombolewa."
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




