Ubalozi wa Burundi nchini China Wafanya Onyesho la Kitamaduni (4)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 29, 2026
Ubalozi wa Burundi nchini China Wafanya Onyesho la Kitamaduni
Kikundi cha sanaa cha Burundi kikitumbuiza ngoma za jadi. (Picha na Wu Qianqian/People's Daily Online)

Jana Jumapili tarehe 28 Juni, Ubalozi wa Jamhuri ya Burundi nchini China ulifanya onyesho la kitamaduni katika Klabu ya Kimataifa ya Beijing ikiwa ni sehemu ya mfululizo wa shughuli za Wiki ya Utamaduni ya Burundi ambayo ilianza rasmi siku hiyo na imepangwa kuendelea hadi Julai Mosi.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Waziri wa Vijana, Michezo na Utamaduni wa Burundi, Lydia Nsekera pamoja na mwakilishi wa nchi mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Afrika, ambaye pia ni Balozi wa Burundi nchini China Telesphore Irambona, miongoni mwa viongozi wengine.

Katika siku hiyo, kikundi cha wasanii wa ngoma ya jadi kutoka Burundi kilitumbuiza nyimbo, ngoma na upigaji ngoma wa jadi, kikionyesha uzuri wa sanaa zake za jadi na ala ya muziki ya kitaifa—Ngoma Takatifu ya Burundi, au Ingoma, huku wakipongezwa kwa makofi mengi kutoka kwa watazamaji.

Ngoma Takatifu ya Burundi iliingizwa kwenye Orodha ya Urithi wa Utamaduni Usioshikika wa Binadamu ya UNESCO mnamo mwaka 2014, na ni ishara ya umoja na mwendelezo wa kihistoria wa watu wa Burundi.

Katika hotuba yake, Balozi Irambona alisema kuwa mawasiliano ya kitamaduni ni muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kirafiki kati ya watu wa China na Afrika, yakiwasaidia kubaini mambo yanayofanana, kupunguza vizuizi na kufanya kazi pamoja kuelekea njia ya kisasa inayoheshimu ustaarabu mbalimbali na kukumbatia tamaduni tofauti.

Wiki hiyo ya Utamaduni ya Burundi nchini China yenye kaulimbiu ya "Ngoma Takatifu ya Burundi (Ingoma) Inapoimarisha Uhusiano wa Kiutamaduni kati ya China na Afrika" inafanyika wakati sawa na Mwaka wa Mawasiliano ya Kitamaduni kati ya Watu wa China na Afrika 2026, na pia maadhimisho ya miaka 70 tangu kuanzishwa rasmi kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na nchi za Afrika. Hivyo, upande wa Burundi unatumai kutumia fursa hiyo kuonyesha zaidi taswira na uzuri ya Burundi kwa ulimwengu.

Akizungumza katika mahojiano na People's Daily Online, Waziri wa Vijana, Michezo na Utamaduni wa Burundi, Lydia Nsekera, alisema kuwa urafiki kati ya China na Burundi una historia ndefu na kwamba Burundi inatazamia mawasiliano ya kitamaduni kati ya nchi hizo mbili, ikitumai kuimarisha ushirikiano na mabadilishano ya uzoefu na upande wa China katika nyanja mbalimbali kama vile maendeleo ya vikundi vya kitaifa vya sanaa na ngoma.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha