Lugha Nyingine
Profesa Mchina aliyekwenda kuhudumu katika maeneo ya vijijini ya Beijing (7)
![]() |
| Li Quansheng akijumuisha uzoefu wake wa kufanya kazi kwa miaka miwili katika Kijiji cha Dongshaoyun, Eneo la Miyun la Beijing kwenye ripoti ya utafiti ya maneno 120,000. (People's Daily Online/Zhang Rong) |
Mwishoni mwa Machi, pande za vilima vinavyozunguka kijiji cha Dongshaoqu katika Mji wa Beijing, China vilikuwa vimefunikwa na michanuo ya maua ya peach na apricot. Hata hivyo, Li Quansheng, katibu wa kwanza wa kijiji hicho, alikuwa na muda mchache wa kufurahia kutazama maua hayo.
Katika umri wa miaka 51, mwembamba, mtu wa maneno kidogo, alikuwa tayari ametumia miaka miwili kwenye kijiji hicho cha amani katika Eneo la Miyun, Beijing. Profesa huyo aliyetumwa kutoka Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing, wanakijiji wanamwita kwa upendo "Mwalimu Li." Muda si mrefu, alikuwa mmoja wao.
Kote China, watu wengi wanajishughulisha na kazi kama hiyo. Wanajulikana kwa majina ya "makatibu wa kwanza"—makada wa kujitolea wanaotumwa kutoka idara za serikali, vyuo vikuu, na mashirika yanayomilikiwa na serikali kwenda vijijini. Dhamira yao ni kusaidia kuendeleza tasnia za vijiji husika na kuboresha maisha ya watu.
"Nilizaliwa kijijini," amesema Li. "Matamanio yangu makubwa daima yamekuwa kusaidia wanakijiji wenzetu kuishi maisha bora."
Darasa la Michezo la Mwalimu Li
Siku ya Li huanza katika shule ya msingi ya kijiji.
Kwa zaidi ya miaka 20, Li amekuwa akifundisha jiaodi, mtindo wa kale wa Kichina wa mchezo wa mieleka, katika Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing. Hata aliwahi kuanzisha mchezo huo wa jadi katika shule nchini Hungary na Poland. Sasa alikuwa akiupeleka kwa watoto wa Dongshaoqu pia.
Karibu na hapo, watoto kumi na wawili walikuwa kimya wakisoma vitabu vya Kiingereza vilivyochangiwa kupitia mawasiliano ya Li na chuo. Guo Hongyan, makamu mkuu wa Shule ya Msingi ya Dongshaoqu ambaye alikulia kijijini hapo na akaamua kubaki, ameielezea hali hiyo kwa ufupi: "Tofauti kubwa kati ya watoto wa mijini na vijijini iko kwenye upana wa upeo wao. Mwalimu Li ameleta mawazo mapya na ulimwengu mpana zaidi kijijini kwetu."
Chakula cha mchana cha kupikwa nyumbani na barabara
Baada ya darasa, Li alinunua samaki freshi na tofu. Alikuwa akielekea nyumbani kwa Diao Shufang mwenye umri wa miaka 81, mjane anayeishi peke yake, ili kumpikia chakula cha mchana.
Li alimsalimia kwa uchangamfu na kwenda moja kwa moja jikoni. Diao aliegemea fremu za mlango, akiongea naye wakati akifanya kazi.
"Shangazi, tunakarabati barabara za kijijini," alisema Li wakati huohuo akipika. "Kufikia Mei, zitakuwa laini zaidi. Kisha utaweza kutoka nje kwa urahisi zaidi."
"Ambacho ni muhimu zaidi kwetu sisi wanakijiji ni barabara," Diao alijibu. "Watoto wangu wana wasiwasi nitaanguka. Mara barabara zitakapokuwa zimekarabatiwa, sitalazimika kukaa ndani tu."
Nyanya, video, na ulimaji wa majira ya mchipuko
Mchana wa siku hiyo, Li alienda kwenye vibanda vya kilimo cha kisasa cha kijani vya kijiji.
Kilimo daima kimekuwa uti wa mgongo wa Dongshaoqu. Nyanya zinazokuzwa hapa ni za kipekee. Hata hivyo, wakulima wengi wana umri zaidi ya miaka 60 na hawana ufahamu wa intaneti, hivyo kupata wanunuzi kwa muda mrefu imekuwa ni changamoto.
Li alikuwa na wazo juu ya changamoto hiyo. Alianza kutengeneza video fupi: picha za ukaribu za nyanya nyororo zikiwa bado kwenye mzabibu, nyuki wakipiga kelele kwa pilika nyingi katikati ya maua… Aliweka klipu hizo mtandaoni. Polepole, zilianza kuvutia ufuatiliaji wa watu.
Jibu la maneno 120,000
Mwisho wa siku, Li alirudi kwenye ofisi yake ndogo. Juu ya meza kulikuwa na ripoti ya utafiti yenye maneno 120,000—miaka miwili ya ziara za bidii kubwa shambani, uchambuzi makini wa matatizo, na takwimu za kina za kijiji.
Muhula wake wa miaka miwili ulikuwa unakaribia kwisha. Alitumaini kukabidhi ripoti hiyo kwa katibu wa kwanza ajaye, ili kazi hiyo iweze kuendelea bila kukatizwa.
"Maua huchanua kila majira ya mchipuko," alisema kwa sauti tulivu ya chini, "lakini kuhakikisha kwamba wanakijiji wetu 1,986 wanaishi maisha bora ni wajibu ambao hauwezi kusubiri hata siku moja."
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




