Lugha Nyingine
Reli mpya ya mwendo-kasi yaunganisha katikati na magharibi mwa China kwa kuhimiza uratibu na maendeleo (3)
![]() |
| Abiria wakiwa wamepanga foleni ili kuingia katika Stesheni ya Reli ya Mashariki ya Xi'an, katika Mkoa wa Shaanxi, kaskazini magharibi mwa China, Juni 30, 2026. (Xinhua/Li Yibo) |
XI'AN - Treni ya mwendo-kasi ya Fuxing imeondoka kutoka Stesheni ya Reli ya Mashariki ya Xi'an iliyofunguliwa hivi karibuni huku treni nyingine ikiondoka kutoka Stesheni ya Reli ya Mashariki ya Shiyan katika upande mwingine jana Jumanne asubuhi, ikionesha kuzinduliwa kwa reli ya mwendo-kasi ya Xi'an-Shiyan, ushoroba mpya mkubwa wa usafiri unaounganisha katikati na magharibi mwa China.
Reli hiyo imesanifiwa mwendo kasi wa treni kufikia kilomita 350 kwa saa na urefu wa jumla wa reli hiyo ni kilomita 257. Reli hiyo inaunganisha Xi'an, mji mkuu wa Mkoa wa Shaanxi, kaskazini magharibi mwa China, na Shiyan katika Mkoa jirani wa Hubei katika eneo la katikati la nchi ya China.
Reli hiyo inaunganishwa na reli ya mwendo-kasi ya Wuhan-Shiyan iliyopo sasa, ikipunguza muda wa usafiri kati ya Xi'an na Wuhan, hadi saa 2 na dakika 41 kutoka saa 4.5 kwenye njia ya awali. Muda wa usafiri kati ya Xi'an na Shiyan umepunguzwa kuwa saa moja tu kutoka saa zaidi ya sita kwenye treni za kawaida.
Wakati wa kipindi cha Mpango wa 15 wa Miaka Mitano wa China (2026-2030), serikali imepanga kuharakisha kazi ya kuhimiza ujenzi wa usafiri na uchukuzi na kukamilisha mfumo wa mambo ya kisasa wa usafiri jumuishi.
Kwa kushinda vizuizi vya mazingira ya asili katika moja ya maeneo yenye utatanishi zaidi ya kijiolojia ya China na kuunganisha sehemu za milimani zilizokuwa zimetengwa hapo kabla na mtandao wa reli ya mwendo-kasi kote nchini, reli hiyo ya Xi'an-Shiyan inatazamiwa kuleta mabadiliko katika usafiri, maendeleo ya viwanda na shughuli za utalii katika eneo kubwa la katikati na magharibi mwa China.
Ujenzi wa reli hiyo ulianza mwaka 2021 kwa jumla ya uwekezaji wa yuan bilioni 47.68 (dola za Marekani karibu bilioni 7). Njia hiyo ya reli inapita Milima ya Qinling, mpaka wa asili kati ya kaskazini na kusini mwa China, na Mto Hanjiang, ambao ni tawi kuu la Mto Changjiang.
Katika miongo kadhaa iliyopita, hali ya kijiografia yenye utatanishi katika sehemu za Milima ya Qinling ilizuia usafiri na mawasiliano ya kiuchumi katika maeneo mengi.
Mao Lei, msanifu mkuu wa mradi huo, ameielezea njia hiyo ya reli kuwa ni reli inayopita kwenye "makumbusho ya jiolojia ya mazingira ya asili" kwani uwiano wa madaraja na mahandaki kwenye njia hiyo unazidi asilimia 90.
Wataalamu wanaona reli hiyo itaimarisha mawasiliano ya kiuchumi kati ya magharibi, katikati na mashariki mwa China, wakati huohuo italeta msukumo mpya kwa maendeleo kwenye Ukanda wa Kiuchumi wa Mto Changjiang.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




