Maadhimisho ya Miaka 64 ya Uhuru wa Burundi Yafanyika Beijing (4)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 03, 2026
Maadhimisho ya Miaka 64 ya Uhuru wa Burundi Yafanyika Beijing
Mwakilishi wa nchi mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Afrika, ambaye pia ni Balozi wa Burundi nchini China Telesphore Irambona, pamoja na Mwakilishi Maalum wa Serikali ya China kwa Mambo ya Afrika, Liu Xianfa wakitoa heshima kwa wageni waalikwa. (Picha na People’s Daily Online)

Sherehe ya kuadhimisha miaka 64 ya uhuru wa Burundi imefanyika katika Hoteli ya China World Beijing Jumanne wiki hii, tarehe 1 Julai na kuhitimisha shughuli za Wiki ya Utamaduni ya Burundi, ambazo ziliandaliwa na Ubalozi wa Jamhuri ya Burundi nchini China tangu Juni 28.

Sherehe hiyo ilihudhuriwa na mwakilishi wa nchi mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Afrika, ambaye pia ni Balozi wa Burundi nchini China Telesphore Irambona, Waziri wa Vijana, Michezo na Utamaduni wa Burundi, Lydia Nsekera, na Mwakilishi Maalum wa Serikali ya China kwa Mambo ya Afrika, Liu Xianfa.

Katika hotuba yake, Balozi Irambona alisema kuwa mwaka huu Burundi inashika uenyekiti wa zamu wa Umoja wa Afrika, ikitokea kwa wakati sawa na Mwaka wa Mawasiliano ya Kitamaduni kati ya Watu wa China na Afrika 2026, na pia maadhimisho ya miaka 70 tangu kuanzishwa rasmi kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na nchi za Afrika.

Balozi huyo amesema kwa sasa, Burundi imepata amani na utulivu tena, na wananchi wake wamejitolea katika kufikia dira yake ya maendeleo ya "Nchi yenye Uchumi Unaoibuka Ifikapo 2040, Nchi Iliyoendelea Ifikapo 2060", ambayo inaendana kwa kiasi kikubwa na "Dira ya Ushirikiano wa China-Afrika 2035", Ajenda ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu 2030, na Ajenda ya AU ya 2063.

Amesema Burundi itategemea kikamilifu juhudi zake yenyewe, na ushirikiano wa kunufaishana na nchi washirika, ikiwemo China, ili kuchochea kufikiwa kwa malengo yake hayo ya maendeleo.

Balozi alibainisha kuwa uhusiano wa kirafiki na kiushirika wa pande mbili kati ya Burundi na China unaendelea kuzidishwa na kuimarika.

Ametumia fursa ya maadhimisho hayo, kuishukuru China kwa dhati kwa uungaji mkono wake kwa Burundi katika nyanja nyingi kama vile siasa, elimu, afya, kilimo, na miundombinu.

Balozi huyo pia amekipongeza Chama cha Kikomunisti cha China kwa maadhimisho yake ya miaka 105 tangu kuanzishwa kwake, na kusifia mafanikio yake makubwa katika kuongoza watu wa China katika muda mrefu uliopita. Balozi huyo pia ameushukuru upande wa China kwa kutoza ushuru sifuri kwa bidhaa zote zinazoingizwa kutoka Burundi, akibainisha kuwa kutokana na sera hiyo, biashara kati ya pande mbili imeongezeka kwa kasi, na amealika pande zote kuendelea kuwekeza nchini Burundi.

Katika hotuba yake, Liu Xianfa alisema kwamba katika kipindi cha miaka 64 tangu Burundi ipate uhuru, serikali na watu wa Burundi wamejitahidi kuchunguza njia ya maendeleo inayolingana na hali halisi ya nchi yao, kujitolea kudumisha amani ya nchi na kuimarisha umoja wa kitaifa, na kupata maendeleo ya haraka ya kiuchumi na kijamii, hali ambayo imeleta mafanikio yenye kuacha alama.

Amesema leo hii, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Evariste Ndayishimiye, serikali na watu wa Burundi wamekuwa wamoja na wakisonga mbele kwa uthabiti kuelekea kutimiza dira ya maendeleo ya nchi. Amesema, China inatakia kwa dhati na inaamini kwamba Burundi itaendelea kupata mafanikio mapya katika safari yake kuelekea maendeleo ya mambo ya kisasa.

Liu alisema, uhusiano wa kirafiki kati ya China na Burundi una historia ndefu, na kwa zaidi ya nusu karne, bila kujali mabadiliko katika hali ya kimataifa, China na Burundi siku zote zimekuwa zikiheshimiana, kushirikiana kwa usawa, na kuungana mkono, na kuwa uthibitisho dhahiri wa ushirikiano wa ngazi ya juu kati ya China na Afrika na kati ya nchi za Dunia ya Kusini.

Amesema chini ya uongozi wa kimkakati wa viongozi wa nchi mbili, uhusiano wa washirika wa kimkakati wa pande zote kati ya China na Burundi unashamiri, na sera ya ushuru sifuri imeingiza nguvu mpya katika ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara wa pande mbili.

Amesema China iko tayari kufanya kazi pamoja na Burundi ili kuchukua sera ya ushuru sifuri kama hatua mpya ya kuanzia, kuimarisha kasi ya ukuaji wa biashara ya pande mbili, kupanua ushirikiano katika nyanja za kilimo na madini, na kuendeleza ushirikiano wa kivitendo wenye ubora wa juu kati ya China na Burundi.

Katika hafla hiyo, Kikundi cha Sanaa za Jadi cha Burundi kilitumbuiza nyimbo, uchezaji na upigaji wa ngoma, kikionesha uzuri wa kipekee wa utamaduni wa jadi wa Burundi kwa wageni waalikwa.

Burundi ilitangaza uhuru wake Julai 1, 1962, ikianzisha Ufalme wa Burundi. Jamhuri ya Burundi ilianzishwa rasmi Novemba 28, 1966. Jamhuri ya Pili ya Burundi ilianzishwa Novemba 1, 1976. Jamhuri ya Tatu ya Burundi ilianzishwa Septemba 3, 1987. Mwezi Septemba 2024, uhusiano kati ya China na Burundi ulipandishwa ngazi hadi kuwa uhusiano wa washirika wa kimkakati wa pande zote, ukiingia kwenye hatua mpya katika uhusiano wa pande mbili.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha