Namibia yafanya maadhimisho ya kwanza kabisa ya Siku ya Kukumbuka Mauaji ya Kimbari

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 29, 2025
Namibia yafanya maadhimisho ya kwanza kabisa ya Siku ya Kukumbuka Mauaji ya Kimbari
Rais Netumbo Nandi-Ndaitwah wa Namibia (kulia) akizungumza katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya Kukumbuka Mauaji ya Kimbari mjini Windhoek, Namibia, Mei 28, 2025. (Picha na Sharon Kavhu/Xinhua)

WINDHOEK - Namibia imefanya maadhimisho ya kwanza kabisa ya Siku ya Kukumbuka Mauaji ya Kimbari kuomboleza watu zaidi ya 100,000 wa Makabila ya Waavaherero na Wanama ambao waliuawa kwa kulengwa makusudi na vikosi vya wakoloni wa Ujerumani kati ya mwaka 1904 na 1908 mjini Windhoek ambapo Rais Netumbo Nandi-Ndaitwah wa nchi hiyo amekumbushia ukatili huo uliofanywa na serikali ya kikoloni ya Wajerumani chini ya sera yake ya kuangamiza na mauaji ya kimbari.

Amesema kwamba watu wengi wa makabila ya Waovaherero na Wanama walilazimishwa kuingia kambi za mateso, ambako walikufa kwa njaa, na mafuvu yao yalipelekwa Ujerumani kwa kile kinachoitwa utafiti wa kisayansi.

Amezihimiza jamii zilizoathirika kuendelea kushirikiana na serikali kutafuta suluhu ya muda mrefu ya mazungumzo kwenye suala la ulipaji fidia na Ujerumani.

Wakati huo huo, Rais Nandi-Ndaitwah ametambua kuwa serikali ya Ujerumani imekubali kuomba radhi kwa umma kutokana na mauaji hayo ya kimbari.

"Pia tunakuwa na faraja kiasi kutokana na ukweli kwamba serikali ya Ujerumani imekubali kuomba radhi kwa jamii zilizoathirika na watu wa Namibia kwa ujumla. Huenda hatutakubaliane juu ya kiasi cha mwisho cha fidia, lakini hiyo ni sehemu ya mazungumzo magumu ambayo tumekuwa tukifanya na Serikali ya Ujerumani tangu 2013," amesema.

Siku hiyo ya Kukumbuka Mauaji ya Kimbari ilianzishwa kufuatia hoja iliyowasilishwa katika Bunge la Taifa la nchi hiyo mwaka 2016, ambayo ilisababisha mchakato wa mashauriano ya nchi nzima kati ya mwaka 2017 na 2020.

Tarehe ya Mei 28 ina umuhimu mkubwa wa kihistoria kwa nchi hiyo, ikiadhimisha siku ya serikali ya kikoloni ya Ujerumani ilipoamuru kufunga kambi za mateso mwaka 1907, ambako kulikomesha mauaji hayo ya kulengwa kwa makusudi na ya kikatili.

Hafla hiyo ya Jumatano ilihudhuriwa na mamia ya watu, wakiwemo wajumbe wa serikali ya Namibia na wanadiplomasia.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha