Mkutano wa 60 wa mwaka wa Kundi la Benki ya Maendeleo ya Afrika yaanza mjini Abidjan

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 29, 2025
Mkutano wa 60 wa mwaka wa Kundi la Benki ya Maendeleo ya Afrika yaanza mjini Abidjan
Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa 60 wa Mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) mjini Abidjan, Ivory Coast, Mei 27, 2025. (Picha na Yvan Sonh/Xinhua)

ABIDJAN - Mkutano wa 60 wa Mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) umefunguliwa juzi Jumanne katika mji mkuu wa kiuchumi wa Ivory Coast, Abidjan, ukihudhuriwa na watu zaidi ya 5,000, wakiwemo wakuu wa nchi na serikali, mawaziri wa fedha, magavana wa benki kuu, viongozi wa kibiashara, wasomi na wawakilishi wa majopo ya washauri bingwa kutoka barani Afrika.

"Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1964, Benki ya Maendeleo ya Afrika imebadilisha kwa kiasi kikubwa hali ya uchumi na jamii ya Afrika," amesema Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast kwenye hafla ya ufunguzi mjini Abidjan.

Ameelezea jukumu muhimu la AfDB katika kuunga mkono maendeleo katika bara zima, akisema kuwa miradi ya ushirikiano kati ya Benki hiyo na Ivory Coast imeongezeka zaidi ya maradufu katika muongo mmoja uliopita. Ouattara amesisitiza kuwa taasisi hiyo ni mshirika mkuu katika kutekeleza mipango ya maendeleo ya kitaifa ya nchi yake.

Amesema, kaulimbiu ya mwaka huu, "Kuufanya Mtaji wa Afrika ufanye Kazi Bora kwa ajili ya Maendeleo ya Afrika," inatoa jukwaa la kutafuta njia za mageuzi na sera zinazolenga kuongeza ufanisi wa rasilimali watu, fedha na biashara ili kuhimiza mabadiliko ya kimuundo ya uchumi wa Bara la Afrika.

Ouattara pia amempongeza Rais wa AfDB Akinwumi Adesina kwa uongozi wake katika kuhimiza maendeleo ya Afrika kupitia mpango wa Benki hiyo wa High 5s: Angaza na Kuipa Nishati Afrika, Lisha Afrika, Fanya Afrika kuwa ya viwanda, Fungamanisha Afrika, na Kuboresha Maisha ya Watu wa Afrika.

Mikutano hiyo itakamilika kesho Ijumaa na jambo muhimu la kufutilia ni uchaguzi wa rais mpya wa AfDB unaofanyika leo Alhamisi ambapo wagombea wake ni: Amadou Hott (Senegal), Samuel Munzele Maimbo (Zambia), Sidi Ould Tah (Mauritania), Abbas Mahamat Tolli (Chad), na Bajabulile Swazi Tshabalala (Afrika Kusini).

Ikiwa ilianzishwa mwaka 1964 huku ikiwa na makao yake makuu mjini Abidjan, dhamira kuu ya Benki ya Maendeleo ya Afrika ni kuhimiza maendeleo endelevu ya kiuchumi na maendeleo ya kijamii katika nchi wanachama za kikanda. China ilianza kuwa nchi mwanachama wa taasisi hiyo mwaka 1985.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha