Marekani yasema Israel imekubali pendekezo la kusimamisha vita kwa muda katika Gaza

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 30, 2025
Marekani yasema Israel imekubali pendekezo la kusimamisha vita kwa muda katika Gaza
Msemaji wa Ikulu ya White House, Karoline Leavitt akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House mjini Washington, D.C., Marekani, Mei 29, 2025. (Xinhua/Hu Yousong)

WASHINGTON - Ikulu ya White House imesema kwamba Israel imetia saini pendekezo la usimamishaji mapigano ya Gaza kwa muda wa siku 60 huku jeshi la Israel likiendelea na operesheni zake za kijeshi katika eneo hilo la vita ambapo Msemaji wa Ikulu hiyo Karoline Leavitt amethibitisha kwenye mkutano na waandishi wa habari kwamba Mjumbe Maalum wa Marekani katika Mashariki ya Kati Steve Witkoff na Rais wa Marekani Donald Trump "wamewasilisha pendekezo hilo la kusimamisha mapigano ambalo Israel imelikubali na kuliunga mkono.

"Israel imetia saini pendekezo hili kabla ya kutumwa kwa Hamas. Ninaweza pia kuthibitisha kwamba majadiliano hayo yanaendelea, na tunatumai kwamba usimamishaji vita mjini Gaza utatokea ili tuweze kurudisha mateka wote nyumbani," amesema Leavitt jana Alhamisi.

"Sitatoa maoni zaidi, kwani tuko katikati ya hili kwa sasa," ameongeza.

Afisa mmoja wa Israel na chanzo cha habari cha Marekani anayejua jambo hilo wamethibitisha kwamba makubaliano hayo pendekezwa si tu yanahusu usimamishaji mapigano kwa siku 60 bali pia mipango ya kuachilia huru mateka 10 walio hai na miili ya mateka 18 waliofariki dunia, shirika la habari la CBS limeripoti.

Hamas imesema siku hiyo ya Alhamisi kwamba uongozi wake umepokea pendekezo hilo jipya la kusimamisha mapigano huko Gaza kutoka kwa Witkoff kupitia wapatanishi na walikuwa wakilisoma.

"Uongozi wa Hamas umepokea pendekezo jipya la Witkoff kutoka kwa wapatanishi na wanalisoma kwa kuwajibika katika namna ambayo inaendana na maslahi ya watu wetu, kutoa msaada, na kufikia usimamishaji vita wa kudumu katika Ukanda wa Gaza," Hamas imesema katika taarifa yake fupi.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha