

Lugha Nyingine
Uzoefu wa China katika kudhibiti jangwa wasaidia maendeleo ya kijani ya Mauritania
![]() |
Mfanyakazi akimwagilia mimea katika Eneo Maalum la Teknolojia ya Kijani la China na Afrika huko Bir El Barka, Mkoa wa Trarza, magharibi mwa Mauritania, Mei 22, 2025. (Xinhua/Si Yuan) |
NOUAKCHOTT - Chini ya jua kali la kuchoma mwili, safu za njia za umwagiliaji zimelala vizuri kwenye eneo karibu lote la mashamba ya mchanga huko Bir El Barka, kijiji katika mkoa wa Trarza, magharibi mwa Mauritania. Miche ya mboga za majani yanachipuka kutoka kwenye mchanga wa manjano.
Karibu na shamba hilo, paneli za nishati ya jua zinabadilisha kwa kasi mwanga wa jua kuwa umeme, ukizipa nishati pampu zinazochota maji chini ya ardhi hadi shambani. Jangwa hilo lililogawanywa, ambalo hapo awali lilikuwa lisilo na tija, sasa lina rangi ya kijani, mandhari dhahiri ya mageuzi.
"Huu si mradi wa muda mfupi wa mandhari bali ni mageuzi endelevu wa kijani," amesema Tourad Medou, mratibu mwenza wa Mradi wa Kielelezo wa Mauritania wa Eneo Maalum la Teknolojia ya Kijani la China na Afrika, huku akitembea kupitia mashambani, bilinganya freshi iliyovunwa ikiwa mkononi.
Medou, ambaye alihitimu shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Hunan nchini China, sasa anafanya kazi katika Wizara ya Mazingira na Maendeleo Endelevu ya Mauritania, yenye jukumu la kuhimiza ushirikiano wa kijani na China.
Nyuma yake, vijana kadhaa wafanyakazi wenyeji walikuwa na pilika nyingi wakilima shamba na kutengeneza njia za umwagiliaji.
Licha ya joto kukaribia nyuzi joto 45, miche ya mboga hizo za majani ilikuwa ikionekana kuwa iliyostawi kijani na kujaa uhai.
"Sikuwahi kufikiria ningekuwa nikikuza mboga katika jangwa," anasema Mohamed Isselmou, fundi wa mfumo wa umwagiliaji wa eneo hilo maalum.
Kwa ushirikiano kati ya Mauritania na China, mradi huo umejengwa na kuungwa mkono na Taasisi ya Ikolojia na Jiografia ya Xinjiang (XIEG), mshirika wa Akademia ya Sayansi ya China (CAS).
Likiwa lilikamilishwa Julai 2024, eneo hilo maalum lenye ukubwa wa hekta 4 lina ukanda wa kuzuia mchanga, ukanda wa bustani, ukanda wa mboga za majani, ukanda wa kukuza malisho, na ukanda wa kufuga kuku.
Bir El Barka iko umbali wa kilomita karibu 70 mashariki mwa Nouakchott, kwenye ukingo wa jangwa. "Tulichagua sehemu karibu na mji mkuu ili kuwezesha kielelezo cha kiufundi na mafunzo na upanuzi katika siku zijazo," anasema Zhou Na, mtaalam wa timu ya utafiti wa jangwa ya XIEG inayofanya kazi kwenye mradi huo.
Likiwa linapatikana katika hali ya hewa ya kitropiki ya jangwa, eneo hilo linakumbwa na ukame, joto kali, dhoruba za mchanga, na kujaa kwa chumvi kwenye udongo kwa muda mrefu. Hakuna malisho ya asili na miundombinu kilimo ilikuwa michache. Eneo hilo bado halijaunganishwa kwenye gridi ya umeme, na maisha ya wenyeji kwa kawaida yamekuwa yakitegemea ufugaji, huku kukiwa hakuna vyanzo endelevu vya mapato.
"Changamoto za kiikolojia na maendeleo zimeingiliana sana hapa. Tunatumai kutafuta muundo wa maendeleo ambao unaweza kubadilika sana kuendana na hali ya hapo na unaweza kutumika chini ya hali hizi za mazingira ya asili." Zhou amesema.
"Ardhi hii ilikuwa ni mchanga uliokuwa ukipotea tu. Hakuna kitu kilichoweza kukua hapa," Medou ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua, akionyesha matuta ya mawe kwa mbali.
Kutokana na uungwaji mkono wa wataalamu wa China na utumiaji wa teknolojia za kudhibiti jangwa za China, zikiwemo za umwagiliaji wa kisasa, fito za nailoni za kuimarisha mchanga, uvutaji maji unaowezeshwa na nguvu ya nishati ya jua, upandaji mimea kwenye mchanga, na uboreshaji wa udongo, mandhari ambayo hapo awali ilikuwa isiyo na tija inabadilika polepole kuwa kijani.
Zhou amesema, teknolojia hizo, ambazo zinatumika sana katika Mkoa unaojiendesha wa Xinjiang, kaskazini magharibi mwa China, zimerekebishwa kabla ya "kutumika" katika mabara mbalimbali ili kuendana na hali ya kienyeji.
Mradi huo tayari umekamilisha kilimo cha majaribio cha karoti, beets, maharagwe ya korongo, na mazao mengine, huku baadhi yao yakifikia hatua za mavuno na kupanda tena, yakiunda msingi wa mzunguko mzuri wa ikolojia.
Eneo Maalum la Teknolojia ya Kijani la China na Afrika ni mradi muhimu wa kielelezo unaoungwa mkono na Mpango wa Ukuta Mkuu wa Kijani wa Afrika, uliozinduliwa mwaka 2007 ili kuunda kizuizi cha ikolojia cha urefu wa kilomita 7,000 kaskazini mwa Afrika na Sahel ili kukabiliana na hali ya kuenea kwa jangwa.
Mauritania, ikiwa ni mwenyekiti wa zamu wa mpango huo, ni mwenyeji wa Sekretarieti ya Ukuta Mkuu wa Kijani wa Afrika mjini Nouakchott, ambayo inaratibu juhudi husika.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma