Afrika Kusini yazindua mpango kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika maeneo ya pwani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 06, 2025
Afrika Kusini yazindua mpango kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika maeneo ya pwani
Mtu akifanya kazi katika kituo cha kuchakata plastiki cha Extrupet mjini Wadeville, karibu na Johannesburg, Afrika Kusini, Juni 5, 2025. (Picha na Shiraaz Mohamed/Xinhua)

JOHANNESBURG – Katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani, Afrika Kusini imetangaza jana Alhamisi mpango wake mpya wa Mwitikio wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi katika Pwani, mpango mkakati wa kuimarisha uhimilivu katika maeneo ya pwani yanayokabiliwa na tishio la tabianchi ambapo Waziri wa Misitu, Uvuvi na Mazingira wa nchi hiyo Dion George amesema mpango huo unaendana na ahadi za Afrika Kusini chini ya Makubaliano ya Paris na kuunga mkono malengo ya uchumi wa baharini ya nchi hiyo wakati huohuo ukilinda sekta muhimu kama utalii na uvuvi.

"Mpango huu unatoa mfumokazi wa kimkakati wa kuongoza juhudi za serikali kuu, za jimbo, na za mitaa katika kujenga uhimilivu wa pwani. Unasisitiza umuhimu wa kulinda jamii, miundombinu, na mifumo ya mazingira ya asili ya pwani kupitia upangaji makini, maendeleo yenye taarifa za hatari, na usimamizi shirikishi," amesema George.

Waziri huyo ametoa wito kwa sekta zote, serikali, makampuni, mashirika ya kiraia na watu binafsi kuungana mkono katika kutekeleza mpango huo.

"Kwa kuoanisha makabiliano ya tabianchi na maendeleo ya kiuchumi, Afrika Kusini inaweza kujenga uchumi wa bluu unaostawi, jumuishi na wenye kuhimili tabianchi ambao unanufaisha vyote watu na sayari ya dunia," amesema.

Pwani ya Afrika Kusini inakabiliwa na changamoto zinazoongezeka za tabianchi ambazo zinatishia jumuiya za pwani, sekta muhimu za kiuchumi, miundombinu muhimu, na mifumo ya ikolojia.

Makadirio ya kisayansi yanaonyesha athari zinazozidi kuwa mbaya kama vile kuongezeka kwa kiwango cha bahari, kuongezeka kwa mmomonyoko wa pwani, na dhoruba kali za mara kwa mara ambazo zinasababisha mafuriko haribifu na kulazimisha kukimbia makazi kwa watu walio katika mazingira hatarishi.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha