

Lugha Nyingine
Ghana yazindua mpango wa taifa wa upandaji miti ili kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani (3)
ACCRA - Rais John Dramani Mahama wa Ghana ametangaza uzinduzi wa mpango wa taifa wa upandaji miti 2025 jana Alhamisi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambapo mpango huo unalenga kupanda miche ya miti milioni 30 ifikapo mwishoni mwa Juni na kushirikisha watoto wenye umri wa kwenda shule katika juhudi za upandaji miti nchini kote kupitia mpango wa "mti mmoja kwa kila mtoto".
Mpango huo utahusisha kila mtoto wa Ghana mwenye umri wa kwenda shule kupanda na kukuza angalau mti mmoja, Mahama amesema. "Hii ni miti ambayo itaimarisha udongo wetu, kupoza miji yetu, kunyonya kaboni, na kurejesha mifumo yetu ya ikolojia iliyoharibiwa."
Rais huyo pia amesisitiza uhusiano kati ya uchafuzi mazingira wa plastiki na ukataji miti, akisema kuwa vyote "vinatokana na sababu halisi ya kuchukulia mazingira kama wazo la baadaye."
Rais Mahama amesema serikali ya nchi hiyo inaanzisha hatua za kukabiliana na uchafuzi wa plastiki na ukataji miti, akiweka mazingira kwenye kiini cha mkakati wa maendeleo wa Ghana.
Ameongeza kuwa serikali imetekeleza sera ya taifa ya usimamizi wa plastiki, ambayo inalazimisha wazalishaji na waagizaji kuwajibika kikamilifu kwa mzunguko wa maisha ya plastiki wanazoziingiza sokoni.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma