

Lugha Nyingine
Teknolojia ya magari yanayojiendesha ya China yaingia katika masoko ya kimataifa
![]() |
Waziri wa Uchukuzi na Huduma za Usafirishaji wa Saudi Arabia Bw. Saleh bin Nasser Al-Jasser (Kulia), akiwa kwenye gari linalojiendesha huko Riyadh, Saudi Arabia, Julai 23. XINHUA |
Matumizi ya kibiashara ya teknolojia ya kisasa ya China ya magari yanayojiendesha yanaenea kote duniani, huku makampuni ya China yakiharakisha kupanua uwepo wao katika masoko ya nje na kupeleka magari hayo.
Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu, wakazi katika baadhi ya miji ya Mashariki ya Kati, wataweza kutumia program za simu za mkononi kwa kuita taxi za magari ya namna hiyo yaliyoundwa na makampuni ya China.
Wataalam wa sekta hiyo wamesema kutumia teknolojia hii kutasaidia kuweka mifumo ya usafiri ya kisasa, salama, yenye ufanisi zaidi na rahisi.
Kampuni kubwa ya teknolojia ya China, Baidu Inc, hivi karibuni ilisaini makubaliano ya ushirikiano wa kimkakati wa miaka mingi na kampuni ya Uber Technologies ya Marekani, ili kupeleka maelfu ya magari yake yanayojiendesha ya Apollo Go kwenye jukwaa la Uber. Makubaliano hayo yanahusisha masoko mengi nje ya Marekani na China bara.
Kwa sasa magari ya Apollo Go yanayojiedesha zaidi 1,000 yamesambazwa katika maeneo mbalimbali duniani. Uwepo wake kimataifa unahusisha miji 15, ikiwa ni pamoja na Dubai na Abu Dhabi nchini Umoja wa Falme za Kiarabu.
Kampuni nyingine ya China ya magari yanayojiendesha, Pony.ai, hivi karibuni ilianza kufanya majaribio ya magari yake nchini Luxembourg kwa ushirikiano na kampuni ya huko ya Emile Weber, kwa kupeleka magari yanayojiendesha na kutumia umeme nchini Luxemburg, na kuharakisha utumiaji wa magari hayo barani Ulaya.
Takwimu kutoka kampuni ya utafiti ya MarketsandMarkets zinaonyesha kuwa, ifikapo mwaka 2030 thamani ya soko la kimataifa la magari yanayojiendesha inatarajiwa kufikia dola bilioni 45.7, ikiongezeka kwa kasi ya asilimia 91.8 kutoka mwaka 2023 hadi mwaka 2030.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma